Leo Septemba 23, 2016 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewasili Wilayani Mafia, Pwani kwaajili ya ziara ya siku mbili ambapo ametoa muda wa siku 10 kwa Taasisi ya Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu kulipa deni la sh. milioni 100 inayodaiwa na Halmashauri ya wilaya ya Mafia kufuatia malimbikizo ya miaka mitatu ya maduhuri yatokanayo na makusanyo yanayofanywa na taasisi hiyo katika maeneo ya hifadhi ya bahari wilayani humo.

Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya hiyo katika ukumbi Caltas ambapo amewataka waandike barua na kuituma leo Taasisi ya Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu kwa njia ya mtandao (email) kuwajulisha kuwa wanatakiwa kulipa deni hilo ndani ya siku 10, Pia wahakikishe wanalipa deni hilo ili Halmashauri iweze kufanya kazi zake vizuri.

Waziri Mkuu amesema Serikali inataka kuona Halmashauri hiyo ikinufaika kutokana na vyanzo vyake vya mapato, hivyo haitakuwa tayari kuona ikihangaika.

Aidha, Waziri Mkuun amesema atafuatilia kuona wajibu wa taasisi hiyo na mipaka yao ikiwa ni pamoja na kujua mapato yatokanayo na shughuli hizo katika maeneo ya hifadhi.

Awali mkuu wa wilaya ya Mafia, Shaib Nnunduma alisema kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili wilaya hiyo ni kutolipwa kwa wakati fedha za maduhuri yatokanayo na makusanyo yanayofanywa na Taasisi ya Hifadhi ya Bahari.

Mkuu huyo wa wilaya ameiomba Serikali kuangalia upya majukumu ya taasisi hiyo na nafasi ya halmashauri katika kuendesha shughuli za uwekezaji pamoja na kupata mapato yatokanayo na shughuli hizo katika maeneo ya hifadhi.

Video: DC Mgandilwa kuimarisha usalama kigamboni, Vituo vya Polisi kujengwa
NEC Yazindua Programu ya utoaji wa elimu ya mpiga kura mashuleni