TAASISI YA KIISLAMU YA IMAMU BUKHARY

TAMKO MAALUM KULAANI KITENDO CHA MWENYEKITI WA CCM MKOA WA DAR ES SALAAM, UMFANANISHA MTUME MUHAMMAD (S.A.W) NA NDUGU EDWARD LOWASSA

“CCM IMUWAJIBISHE NDUGU MADABIDA ILI KUZUIA MACHAFUKO YA KIIMANI NCHINI”

Ndugu Wanahabari,

Mnamo Siku ya Jumamosi tarehe 27.06.2015, mtangaza nia ya urais kupitia CCM, ndugu Edward Lowassa, alifika katika viwanja vya CCM Mkoa wa Dar es Salaam ili kutafuta wadhamini, hotuba kadhaa zilitolewa kabla ya mtangaza nia huyo kuzungumza.

Miongoni mwa waliotoa hotuba ni ndugu Ramadhani Madabida ambaye hatujui kwa malengo gani aliamua kumdhalilisha Mtume Muhammad (S.A.W) kwa kumfananisha na ndugu Edward Lowassa.

Ndugu Wanahabari,

Kufuatia kikao cha wana taasisi kilichoketi kwa dharura tarehe 29/6/2015 Siku ya Jumatatu tumeamua kutamka yafuatayo:

(1) Edward Lowassa hana sifa za kufananishwa na Mtume Muhammad (S.A.W), kiongozi ambaye amejaa maadili mema ambayo Lowassa anaweza kupimwa na kulingana naye. Kitendo cha kumfananisha Mtume Muhammad (S.A.W) na Lowassa ni kumdhalilisha, jambo ambalo Waislamu hatulikubali na kamwe hatuliungi mkono na tunalilaani kwa nguvu zote na kuwataka Waislamu kote nchini kuikataa dhana hiyo.

(2) Katika hatua za awali tunakitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumuwajibisha ndugu Madabida kwa kumvua cheo chake cha Uenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam ili Waislamu tujiridhishe kwamba yale si maneno ya CCM bali ni ya Madabida yeye kama yeye.

(3) Tunamtaka mtangaza nia, Ndugu Edward Lowassa, akane hadharani kwamba yeye hakumtuma Madabida amfananishe na Mtume Muhammad (S.A.W) kwani kitendo cha yeye kubakia kimya siku ile, kinaonyesha kuwa yeye ndiye aliyemtuma kufanya hivyo kwa kuhisi kuwa sifa hizo za kufanana na Mtume Muhammad (SAW) zitavuta hisia za Waislamu walio wengi katika hiyo safari yake anayoiita ya matumaini.

Sisi hatuamini kuwa Ndugu Lowassa ni mteule kwa kiwango cha kufananishwa na Nabii wa Mwenyezi Mungu Mtume Muhammad (SAW) ambaye kutomuamini tu kunamfanya mtu kutohesabika kuwa Mwislamu. Ni katika hali hiyo sisi hatuamini kuwa hata katika hizo mbio za kugombea Urais mtu ambaye chaguo lake ni mtangazania mwingine ghairi ya Lowassa hatokuwa na dhambi kwa Mwenyezi Mungu.

(4) Tunamkumbusha mtangazania, Edward Lowassa, pamoja na michango yake mingi anayowapa baadhi ya Waislamu, bado Waislamu wanautazama mkataba kati ya Serikali na Makanisa (MOU) ambao yeye Lowassa alikuwa ndiye mbunifu na mfanikishaji wake, kama zilikuwa ni hila na upendeleo wa makusudi wa kidini.

(5) Tunawaomba Waislamu wote kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho tunakisubiri Chama Cha Mapinduzi (CCM) kichukue hatua stahiki kwa kumvua ndugu Madabida vyeo vyake vyote kichama na kutoa angalizo kwa wana CCM wengine wasiyachezee maandiko matakatifu ya Quraan na kiongozi wetu mtukufu, Mtume Muhammad (S.A.W) kwani hasira za Waislamu ni kali sana pale anapodhalilishwa kiongozi wao.

(6) Tunamtaka ndugu Ramadhani Madabida atamke hadharani kufuta kauli yake ya kumfananisha Mtume Muhammad (S.A.W) na Lowassa, na asirudie tena kutumia Aya za Mwenyezi Mungu (Quraan) ili kumfurahisha Ndugu Lowasa, lakini pia asirudie tena kuichezea Quraan kwa kutunga tafsiri potovu ili kumpumbaza Ndugu Lowassa.

(7) Tunaiomba Serikali haswa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viwe makini sana na watu wanaotaka kuvunja amani ya nchi kwa kuwaudhi na kuwatia hasira waumini wa dini fulani, kwani siku zote mlipuko wa kiimani ni hatari sana. Na katika hili la kumdhalilisha Mtume Muhammad (SAW) tuna hakika Waislamu wote kwa madhehebu zatu tunaungana pamoja.

Ahsanteni sana.

………………………
Shk Khalifa Khamis
MWENYEKITI
TAASISI YA KIISLAMU YA IMAMU BUKHARI

Mama Wa Chris Brown Amponza Mkwewe
Blatter: Nitakapoingia Peponi Ndipo Mtaamini Sikutafuna Rushwa