Serikali imezitaka Taasisi za umma zinazotumia mkaa na kuni kubadilishiwa matumizi na kutumia gesi katika shughuli zake ili kusaidia katika uhifadhi wa mazingira ambao umekuwa tishio.

Hayo yamesemwa mapema hii leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira. January Makamba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa kumekuwa na jitihada mbalimbali katika kutatua tatizo la matumizi ya nishati ya mkaa na kuni, ili kuweka mazingira safi kwa kutunza misitu na kuepusha ukataji wa miti ovyo.

“Kama mnavyofahamu asilimia 90 ya Watanzania wanatumia mkaa na kuni kama nishati ya kupikia na mwanga, hii inasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira kwa sehemu za vijijini ambapo shughuli ya utengenezaji wa nishati hii hufanyika”. amesema Makamba.

Aidha, katika ripoti ya pili ya mazingira ya mwaka 2014 imeonyesha kuwa Jiji la Dar es salaam pekee linatumia wastani wa tani 500,000 ya nishati ya mkaa kila mwaka na mahitaji haya yanaongezeka kila kukicha.

Kwa mujibu wa taarifa ya Taifa ya ufuatiliaji na tathimini ya Rasilimali za misitu nchini, imeonyesha kiasi cha ekari milioni moja au hekta 372,000 zinaharibika kila mwaka  kiasi ambacho ni kiwango kikubwa cha uharibifu wa misitu.

Hata hivyo, Makamba amezitaja  baadhi ya taasisi hizo ambazo mara nyingi zinatumia kuni ili kupata nishati ya kupikia chakula kuwa ni pamoja na Shule mbalimbali nchini, Magereza, Majeshi, Hospitali, na Vyuo mbalimbali.

 

Video: Sumaye afunguka mazito kuhusu Wema Sepetu
Dkt. Mwakyembe ajitosa kutatua kero za BFT