Naibu Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza, leo katika eneo la Bunge jijini Dodoma, amemkabidhi Peter Mollel maarufu kama ‘Pierre Liqud’ tiketi ya usafiri wa ndege ya kwenda na kurudi nchini Misri kushuhudia michuano ya kombe la Mataifa Huru Barani Afrika (AFCON).

Tiketi hiyo imedhaminiwa na Mradi wa Utambuzi wa wasanii wa Sanaa za Ufundi (TACIP), ambapo tayari Pierre ameshatambuliwa na Mradi huo na kusajiliwa.

Akizungumza wakati wa kukabidhi tiketi hiyo, Mtendaji Mkuu wa Mradi wa TACIP, ambaye ni Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi (TAFCA), Adrian Nyangamalle amesema kuwa sababu kuu iliyowafanya wamdhamini Pierre ni kwakuwa yeye ni msanii wa Sanaa za Ufundi.

“Tumeamua kudhamini safari ya Pierre kwa sababu ni msanii wa sanaa za ufundi, kama tunavyofahamu Pierre ni fundi seremala na tayari ameshasajiliwa na TACIP,” amesema Nyangamalle.

Kabla ya kumkabidhi tiketi hiyo Naibu Waziri Shonza amemwambia Pierre aendelee na uhamasishaji hata atakapofika jijini Cairo nchini Misri.

Aidha, Mbunge William Ngeleja, ambaye ni mratibu wa timu ya michezo ya bunge amesema kuwa safari ya kuelekea Misri kwa ajili ya kuhamasisha ushindi wa Taifa Stars itaanza kesho na kwamba anaamini uwepo wa Pierre ambaye ameungwa mkono na TACIP ni chachu kwa mashabiki wote nchini.

Hatua ya TACIP kumpa tiketi Pierre ni kutimiza ahadi iliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ya kuhakikisha msanii huyo anakuwa sehemu ya timu ya wahamasishaji watakaoenda nchini Misri kushuhudua ushiriki wa Taifa Stars AFCON.

Naye Pierre baada ya kukabidhiwa tiketi hiyo hakusita kutoa shukurani zake za dhati kwa Waziri Mkuu kwa kuanzisha safari yake ya kwenda Misri pamoja na mradi wa TACIP ambao umejitolea kudhamini safari yake.

Taifa Stars inashiriki AFCON ikiwa imepangwa kundi C ikiwa na timu za Algeria, Kenya na Senegal. Tanzania imefuzu kwa mara ya pili baada ya kufikia hatua hiyo kwa mara ya mwisho 1980.

 

 

Mwakyembe amfungia bondia aliyesalimu amri ulingoni
Mwanaume aliyejifanya mwanamke atupwa selo ya kike