Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imetakiwa kufanya kazi zenye tija kwa jamii na kutoa ushauri wa kisayansi namna ya kuhakikisha sekta ya uvuvi inakua na kusaidia watanzania katika masuala ya uvuvi

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amebainisha hayo wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika makao makuu ya taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa TAFIRI inategemewa katika kufanya tafiti za uvuvi kwa manufaaa ya sasa na yajayo na kuwafanya wavuvi kuwa na kipato endelevu ili shughuli hiyo ifanywe kitaalamu.

Aidha, amepongeza Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH), ambapo umewezesha kujengwa kwa jengo la maabara ya TAFIRI ambalo litaongeza wigo katika kufanya tafiti za uvuvi hapa nchini.

Amefafanua kuwa SWIOFISH imekuwa ikifanya kazi ya msingi na muhimu nje ya nchi na kuhakikisha fedha ambazo zimetolewa na Benki ya Dunia katika mradi huo zinasimamiwa vyema na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI Dkt. Ishmael Kimirei amemwambia Waziri Ndaki juu ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo zikiwemo za vifaa vya maabara baada ya jengo la maabara kukamilika ambapo amesema vifaa hivyo vinagharimu Shilingi Bilioni 1.5.

Kutokana na ukosefu wa vifaa vya maabara, Waziri Ndaki amemhakikishia mkurugenzi huyo kuwa, ataliwekea uzito jambo hilo kuanzia sasa na mwaka ujao wa fedha ili vipatikane vifaa hivyo na jengo hilo lifanye kazi ya utafiti pekee badala ya kuwa na vyumba vya ofisi.

Naye Mratibu wa mradi wa SWIOFISH Bw. Nichrous Mlalila amesema mradi huo wa miaka sita hapa nchini unaotarajia kufikia tamati mwezi Septemba mwaka 2022, umefadhiliwa na Benki ya Dunia na lengo la mradi ni kusimamia masuala ya uvuvi kuanzia ngazi ya utawala hadi kwa wavuvi pamoja na ushirikiano kwa kikanda katika kuhakikisha unaboresha mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya siku moja katika makao makuu ya taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam na kuwataka wafanyakazi hao kufanya kazi yenye tija kwa jamii kupitia sekta ya uvuvi.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei akifafanua namna taasisi hiyo inavyokabiliwa na changamoto ya vifaa vya maabara vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.5 mara baada ya jengo la maabara kukamilika. Dkt. Kimirei amebainisha hayo wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki aliyofanya katika makao makuu ya taasisi hiyo. 
Mratibu wa Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi Bw. Nichrous Mlalila akifafanua namna mradi huo wa miaka sita hapa nchini unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, ulivyoweza kuleta tija katika sekta ya uvuvi nchini kupitia tafiti na elimu. 
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), akikagua jengo la maabara la Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) lililojengwa kupitia Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH), ambapo Waziri Ndaki amesema atahakikisha jengo hilo linapata vifaa vya maabara vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.5 ili lifanye kazi iliyokususdiwa.

Young Africans yanoa makali ya ushambuliaji
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Septemba 7, 2021