Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesitisha ratiba ya kufanya mikutano yake ya ndani na ya hadhara, ikiwa ni sehemu ya hatua za kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya corona (Covid-19).

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema kuwa chama hicho kimechukua hatua hiyo kutekeleza maagizo ya Rais John Magufuli aliyoyatoa jana alipokuwa akikagua Mradi wa Barabara ya Juu (Interchange) ya Ubungo jijini Dar es Salaam, alipowataka Watanzania kuchukua tahadhari dhidi ya virusi hivyo.

Polepole ameyasema hayo leo, Machi 17, 2020 katika ofisi ndogo za makao makuu ya chama hicho, Lumumba jijini Dar es Salaam. Amefafanua kuwa ratiba ya viongozi wa chama hicho kuzunguka maeneo mbalimbali nchini kufanya mikutano ya ndani na ya nje imesitishwa.

“Ziara za viongozi zilizokuwa zifanyike nchi nzima zimesitishwa hadi Serikali itakapotoa maelekezo zaidi,” amesema Polepole.

“Vikao vitakavyoendelea ni vile ambavyo vilikuwa kwenye kalenda ambavyo sio mikusanyiko, kama kikao cha Halmashauri Kuu,” aliongeza.

Aidha, ameeleza kuwa chama hicho kitasambaza dawa maalum kwenye ofisi zake nchini kama hatua ya kujikinga na virusi vya corona.

Ametoa wito kwa vyama vingine vya siasa kuiga hatua walizochukua ili kusaidia kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Jana, Tanzania ilitangaza kuwa na kisa cha kwanza cha virusi vya corona. Waziri wa Afya, aendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto alisema kuwa mwanamke Mtanzania mwenye umri wa miaka 46, aliyekuwa anasafiri kutoka nchini Ubelgiji alibainika kuwa ameathirika. Aliingia nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akitokea nchini Ubelgiji.

HOFU YA CORONA: Wafungwa 1,350 watoroka, wateka askari (Video)
RC Arusha ataja mtandao waliokutana na dereva aliyembeba mgonjwa wa Corona

Comments

comments