Timu ya Taifa ya Tanzania inatarajiwa kushuka dimbani Jumapili ya Machi 24, 2019 kwenye uwanja wa taifa, dhidi ya Uganda mchezo ambao ni muhimu kwa Stars kushinda lakini hiyo haitoshi pekee kufanya timu hiyo ifuzu AFCON 2019 nchini Misri, bali itategemea matokeo ya Cape Verde na Lesotho.

Wakati ambao Stars itakuwa inacheza na Uganda Uwanja wa Taifa maarufu kwa Mkapa, Cape Verde wao watakuwa nyumbani mjini Praia kwenye uwanja wa Nacional de Cabo Verde wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 15,000 wakicheza na Lesotho ambao wanahitaji ushindi pekee ili wafuzu bila kujali Tanzania na Uganda zitapata matokeo gani.

Hili linakuja kutokana na Lesotho kuwa na pointi 5 sawa na Tanzania lakini endapo timu zote zinapata ushindi Lesotho inakuwa na faida ya kufuzu na kuiacha Tanzania kutokana na Lesotho kulazimisha sare ya 1-1 kwenye mechi na Tanzania iliyopigwa Juni 10, 2017 kwenye uwanja wa Azam Complex na kisha kushinda 1-0 kwenye mchezo wa marudiano uliopigwa Novemba 18, 2018 huko Lesotho.

Hata hivyo Kundi L ni moja ya makundi yenye mvuto zaidi kutokana na namna lilivyo, ambapo Cape Verde hawezi kuwa mnyonge kwa Lesotho kutokana na yeye kuwa na nafasi ya kufuzu endapo atashinda huku Taifa Stars ikifungwa au kutoa sare na Uganda.

Katika mechi ya kwanza iliyozikutanisha Cape Verde na Lesotho timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, mchezo ambao ulipigwa Septemba 9, 2018 huko Lesotho.

Hili sio jambo geni kwenye soka kwa timu mbili kuwania nafasi moja kwenye mechi ya mwisho ya makundi. Jumamosi iliyopita ya Machi 16, 2019 Watanzania walifurahia ushindi wa 2-1 wa Simba na kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku wakiwaacha AS Vita na JS Saoura wakiumia kwa kukosa nafasi.

JS Sauora walihitaji sare tu kutoka katika mechi ya Simba na Vita ili wao wafuzu katika robo fainali licha ya kuwa walishafungwa na Al Ahly. Katika dakika ya 90 Mzambia Clatous Chama alikata matumaini ya mashabiki wa soka wa Algeria na DR Congo kwa kufunga bao lililoibeba Simba

Miradi 500 ya maji kusambazwa nchi nzima
Mwanaume awaua wanaye watatu kisa mkewe amemuudhi