Baada ya Rais Samia kupitia Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kutangaza kiasi cha Shilingi Milioni 500 kama zawadi kwa Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ endapo itafuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’, Mastaa wa kikosi cha timu hiyo wameapa kuhakikisha wanapambana kufa na kupona ili kuifunga Uganda katika mchezo wa ugenini na nyumbani.

Kikosi cha Stars kwa sasa kipo jijini Ismailia nchini Misri kikijiandaa na michezo miwili ya kusaka tiketi ya kufuzu Fainali za ‘AFCON 2023’ ambazo zinatarajiwa kufanyika nchini Ivory Coast.

Mchezo wa kwanza baina ya timu hizo unatarajiwa kupigwa keshokutwa Ijumaa (Machi 24), mwaka huu kabla ya mchezo wa marudiano ambao unatarajiwa kupigwa Machi 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Mlinda Lango wa Taifa Stars Aishi Manula amesema: “Tumefika katika mazingira mazuri na kila mchezaji anaonyesha kuwa na ari ya kuutaka mchezo huu, Uganda ni timu ngumu hivyo ni wazi hautakuwa mchezo rahisi lakini tunataka kuhakikisha tunafanikisha hilo.”

“Tulikuwa tunasubiri sehemu ya wenzetu ambao bado walikuwa hawajawasili kutokana na majukumu ya timu zao naamini wote kwa pamoja tukikamilika tutakuwa na tayari kuzungumza kiufundi.”

Taifa Stars iliyojikusanyia alama 01 hadi sasa, inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi F ikitanguliwa na Algeria yenye alama 06, huku Niger ikiwa nafasi ya pili kwa kufikisha alama 02 na Uganda inaburuza mkia ikiwa na alama 01.

Young Africans yajipongeza usajili wa Musonda
Shambulio lauwa 41, idadi kubwa Wanawake, Watoto