Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” inaendelea na maandalizi yake ya mchezo wa kuwania tiketi ya kufuzu Afcon 2019 dhidi ya Lesotho utakaochezwa Novemba 18, 2018 Maseru, Lesotho.

Taifa Stars imeweka kambi nchini Afrika kusini kujiandaa na mchezo huo ambao una umuhimu mkubwa katika kufanikisha mpango wa kusaka tiketi ya kutinga kwenye fainai hizo, endapo itachomoza na ushindi wa aina yoyote.

Hata hivyo taarifa zilizotolewa leo mchana na mkuu wa idara ya habari na mawasilino wa shirikisho la soka nchini TFF zimeeleza kuwa, mlinda mlango wa Young Africans Beno Kakolanya na mshambuliaji wa Azam FC Yahya Zayed walikosa mazoezi ya leo baada ya kuumia.

“Bahati mbaya katika mazoezi hayo, kipa Beno Kakolanya na mshambuliaji Yahya Zayed walipumzishwa baada ya kugongana, ingawa taarifa ya madaktari inasema wachezaji hao wataendelea na mazoezi kuanzia kesho.” Alisema Ndimbo

Katika hatua nyingine wachezaji wanaocheza nje wataanza kuripoti kambini hapo Jumapili Novemba 11,2018 na wanaotarajiwa kuanza kuwasili ni Ramadhan Kessy (Nkamia,Zambia), Himid Mao (Petrojet,Misri), Rashid Mandawa (BDF,Botswana) na Abdi Banda (Baroka, Afrika Kusini) huku waliosalia wataripoti kuanzia Novemba 12.

Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde Oktoba 16 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Taifa Stars sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi L kuwania tiketi ya Cameroon mwakani, ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi nne, ikifungwa moja na sare mbili.

Uganda ambayo siku hiyo iliifunga tena Lesotho 2-0 mjini Maseru, ndiyo inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10 za mechi nne, wakati Cape Verde inabaki na pointi zake nne katika nafasi ya tatu. Lesotho ndiyo inashika mkia kwa pointi zake mbili.

Taifa Stars itahitimisha mechi zake za Kundi L kwa kumenyana na Uganda Machi 22 mwakani, miezi miwili tu kabla ya kuanza kwa AFCON ya mwakani.

GGM yalalamika watoto kuvamia mgodini
Ujerumani yatonesha kidonda cha Wayahudi