Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro tayari imewasili salama nchini Uturuki katika mji wa Kartepe – Kocael leo mchana, tayari kwa kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo dhidi ya Nigeria kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika mwaka 2017.

Msafara wa Taifa Stars uliopoa nchini Uturuki unaongozwa na mjumbe wa kamati ya Utendaji ya TFF, Ahmed Mgoyi ukijumuisha benchi la ufundi 7 na wachezaji 21 umefikia katika hoteli ya Green Park Kartepe, ambapo leo jioni timu inatarajiwa kuanza mazoezi.

Kocha Mkuuu wa Taifa Stars Charles Mkwasa mara baada ya kufika katika eneo la kambi, amesema mazingira ya kambi ni mazuri na sasa vijana watapata nafasi nzuri ya kufanya mazoezi na kujiandaa vizuri kwa mchezo dhidi ya Nigeria.

Mkwasa amesema ana imani yeye na benchi lake la ufundi, wataandaa vijana kufanya vizuri kwa mchezo huo wa Septemba 5, 2015 na kuomba watanzania kuwaspoti katika maandalizi hayo kuelekea kwenye mchezo wenyewe.

Kwa mujibu wa ratiba ya kocha Mkwasa, timu itakua ikifanya mazoezi kutwa mara mbili kila siku uwanjani, na kutumia vifaa vya mazoezi viliyopo katika hoteli waliyofikia kuhakikisha timu ikirejea inakuwa katika hali nzuri ya kufanya vizuri zaidi.

Stars inatarajia kucheza michezo miwiliya kirafiki katika wiki moja ya kambi nchini Uturuki, kabla ya kurejea jijini Dar es salaam kupamabana na Nigeria.

U15 Yaingia Kambini
Bondia Francis Cheka Kupanda Uliongo Wa Manchester