Mmiliki wa Klabu ya Chelsea amepanga kufanya mabadiliko makubwa baada kuboronga huku mipango yake ikifeli msimu huu licha ya kufanya kufuru kwenye usajili.

Kwa mujibu wa ripoti bosi huyo ambaye ni mfanyabiashara mkubwa kutoka Marekani, yupo mbioni kumteua mtendaji mkuu mpya atakayesimamia masuala ya klabu.

Mazungumzo kati ya Boehly na Chris Jurasek yamekwenda vizuri na wakati wowote watamtangaza kuwa mtendaji mkuu wa klabu ya Chelsea kwa mujibu ripoti. Aidha, Jurasek bado ataendelea kuwa mtendaji mkuu wa kampuni nyingine ya kibiashara.

Vilevile imethibitishwa kwamba Jurasek atasimamia madili yote ya matangazo ya klabu, lakini gazeti la Times limeripoti uteuzi unaokaribia wa Jurasek umezua hofu kwani ana majukumu mengine ya kibiashara katika kampuni nyingine.

Huu ni msimu wake wa kwanza Boehly ambaye amepitia kipindi kigumu huku The Blues ikijikita katika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Chelsea ilipata ushindi kwa mara ya kwanza dhidi ya Bournemouth wikiendi iliyopita chini ya kocha wa mpito Frank Lampard licha ya tajiri huyo kutumia Pauni 600 milioni katika usajili wa madirisha mawili yaliyopita.

Vile vile Chelsea bado haijathibitisha kuwa imepata kocha mkuu mpya huku Mauricio Pochettino akihusishwa, lakini Lampard ameendelea kuwa kocha wa mpito huku wakiwa wamebakiza mechi nne msimu umalizike.

Boehly alimteua Graham Potter baada ya kumtimua Thomas Tuchel, Septemba mwaka jana lakini kocha huyo wa zamani wa Brighton alidumu kwa muda mfupi.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Mei 14, 2023
Agizo la Waziri Mkuu: Hakuna vifo, mifugo iliyouawa