Watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wametakiwa kujitathmini mapema na ‘majipu’ kujisalimisha mapema kabla ya kutumbuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwani yanafahamika.

Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki alipohudhuria ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa viongozi wa taasisi hiyo.

Aidha, Waziri Kairuki aliwataka watumishi wote kuwasilisha taarifa za mali zao kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki, ili wote waliozipata kwa udanganyifu wabainike.

“Niliposikia mnataja majina yenu wakati wa kujitambulisha, nilikuwa nafurahi sana kwani wengi wenu nawajua na nina taarifa zenu. Haiwezekani wewe mtu mmoja watu wengi wawe wanakuongelea vibaya. Msifikiri majipu humu (Takukuru) hakuna, yapo na nawahakikishia tutayatumbua tu,” alisema Waziri Kairuki.

Aliwatahadharishwa watumishi hao kuwa endapo watasubiri hadi watumbuliwe, hali itakuwa mbaya zaidi kwa kuzingatia kuwa Taasisi hiyo iko chini ya Ofisi ya Rais.

Waziri Kairuki alisisitiza kuwa Serikali itaisafisha Taasisi hiyo hata ikiwa ni kuwafukuza watumishi wake wote endapo watabainika kuwa hawakufuata maadili ya kazi zao ikiwa ni pamoja na kujihusisha na Rushwa.

“Tutasafisha nawahakikishia hata ikibidi kuanza upya, ikitulazimu pia kufukuza wote ikithibitika mnakwenda kinyume na maadili yenu tutawafukuza ila hatutamwonea mtu, kwani wako watu wengi wenye sifa wanaotaka kufanya kazi,” anakaririwa.

Desemba mwaka jana, Rais John Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah na baadae kumteua Valentino Mlowola kukaimu nafasi hiyo.

Tanzia: Msanii Joni Woka afariki
Fahamu Kiasi cha Mshahara na Posho anazolipwa Rais Barack Obama