Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Njombe imejipanga kikamilifu kupambana na kukabiliana na vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa katika ngazi za mitaa, vijiji, wajumbe wa serikali za vijiji pamoja na kamati za serikali za mitaa.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Njombe, Charles Mulebya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa uzoefu unaonyesha kuwa mchakato wa kuwapata viongozi wengi huwa unagubikwa na vitendo vya rushwa ndani ya vyama vyao wakati wa kura za maoni.

Amesema kuwa Takukuru mkoa wa Njombe imejipanga vyema kukabiliana na vitendo vyovyote vinavyokatazwa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi na kwa mujibu wa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007, hivyo atakaye bainika hatua za kisheria zitachukuliwa mara moja.

Aidha, amewakumbusha wananchi mkoani Njombe kuwa wanayo haki na wajibu wa kikatiba kuchagua au kuchaguliwa kwa mujibu wa sheria za nchi na vyama vya siasa.

“Takukuru inawakumbusha wananchi wa mkoa wa Njombe kwamba mnayo haki na wajibu wa kikatiba wa kuchagua au kuchaguliwa kwa mujibu wa sheria za nchi na zile za vyama vya siasa. hakuna chama cha siasa ambacho katiba yake inaeleza kuwa viongozi ndani ya vyama watapatikana kwa njia za rushwa,”amesema Mulebya

Kwa upande wake Katibu Muenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Njombe, Erasto Ngole ameahidi kutokuwepo kwa vitendo vyovyote vitakavyo ashiria rushwa ndani ya chama hicho.

Naye Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Njombe, Alatanga Nyagawa amesema kuwa suala la Rushwa huondoa ustaarabu wa watanzania pamoja na siasa za nchi hivyo ameunga mkono wito wa taasisi hiyo ya kuzuia na kupambana na rushwa mkoani Njombe.

Video: Zitto ajibu hoja tatu za Msajili, CUF wampokonya Maalim Seif ofisi Zanzibar
Rais Felix Tshisekedi wa Congo DR kufanya ziara nchini Marekani