Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), imeanza kuwachunguza na kuwahoji wabunge wote waliotajwa katika tuhuma za kupokea rushwa kutoka kwa mashirika ya umma.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola amesema kuwa taasisi hiyo imechukua hatua ya kumchunguza kila mbunge aliyetajwa ikiwa ni pamoja na mashirika ya umma yaliyohusishwa.

“Sisi tunachunguza tuhuma zote zinazohusiana na rushwa, kwa maana hiyo tunawachunguza wabunge wote waliotajwa,” alisema Mlowola.

Taasisi hiyo imechukua uamuzi huo ikiwa ni siku chache baada ya kuibuka tuhuma nzito za rushwa dhidi ya wabunge wa kamati mbalimbali huku Spika wa Bunge, Job Ndugai akichukua hatua ya kufanya mabadiliko makubwa ya wajumbe wa kamati hizo. Baadhi ya wabunge akiwemo Zitto Kabwe (Kigoma Mjini) na Hussein Bashe (Nzega Mjini) wakitangaza kujiulu katika nafasi zao kwenye kama wajumbe wa kamati hizo wakishinikiza kufanyika kwa uchunguzi na hatua stahiki kuchukuliwa kwa watakaobainika.

Mashirika ya umma yaliyohusishwa na tuhuma za kuwapa rushwa baadhi ya wajumbe wa Kamati za Bunge ni pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).

Zitto Kabwe ameipongeza Takukuru kwa hatua iliyochukua dhidi ya tuhuma hizo akidai kuwa itapelekea ukweli kujulikana.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Zitto ameandika:

“Ni hatua muhimu kwamba TAKUKURU imeanza uchunguzi dhidi ya tuhuma za rushwa kwa Wabunge. Ni hatua kubwa itakayopelekea ukweli kujulikana na watakaokutwa na makosa kuchukuliwa hatua stahiki. Uchunguzi wa vyombo vya dola ni moja ya njia mwafaka ya kuhakikisha kila lisemwalo linakuwa na ukweli na pale ambapo suala limezushwa tu itajulikana na wazushaji hatimaye wataacha. Pale ambapo itakuwa ni kweli na hatua zikachukuliwa tabia za namna hii zitakoma. Bila uchunguzi wa kina Bunge litaendelea kugubikwa na kashfa hizi kwa ukweli au kwa hisia. Hatua iliyochukuliwa na TAKUKURU ni kubwa na ya kuungwa mkono kwa dhati.”

 

Afungwa Maisha Jela kwa Kunajisi
Marekebisho Ya Ratiba Ya Vodacom Premiership