Upatikanaji wa takwimu sahihi za Watu wenye ulemavu umetajwa kusaidia kuwezesha kutungwa kwa sera wakilishi na kupima utekelezaji wa malengo mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Wazri Mku Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene ameyasema hayo katika Kongamano la kuwajengea uelewa Watu wenye ulemavu, kuhusu Sensa ya Watu na makazi ya mwaka 2022 kwa .

Amesema, kwa mujibu wa pango wa tatu wa maendeleo wa miaka mitano (FYDP III) na malengo ya maendeleo endelevu (SDG), imeweka mkazo katika kuhakikisha Watu wenye ulemavu sio tu wanakuwa sehemu ya mipango ya maendeleo ya nchi bali wanapewa kila fursa za kujiendeleza katika nyanja zote za maendeleo kama wananchi wengine.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Wazri Mku Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene.

“Ili kuhakikisha jamii ya Watu wenye ulemavu wanakuwa sehemu ya mchakato mzima wa Sensa ya Watu na makazi, Serikali imezingatia ushiriki wao katika hatua zote za utekelezaji wa zoezi hili la kitaifa na ushiriki wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu nchini (SHIVYAWATA), ni ishara ya ujumuishaji huo,” amesema Waziri.

Simbachawene ambaye alikua akiyasema hayo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pia ameitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bara, na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar kuendelea kuboresha mbinu za ukusanyaji wa taarifa za hali ya ulemavu nchini, kushirikiana na taasisi zinazojihusisha na Watu wenye ulemavu ili kuwatambua na kuwahudumia.

“Ofisi za takwimu ziendelee kujumuisha maswali yanayolenga kupata taarifa za hali ya ulemavu nchini kwenye tafiti mbalimbali zinazofanywa na Ofisi hizo na Ofisi ya Waziri Mkuu ione uwezekano wa kuanzisha mfumo wa Kiutawala wa Kukusanya Taarifa za Hali ya Ulemavu Nchini,” alisisitiza Simbachawene.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali watu wenye ulemavu akisema watahakikisha Taifa linakuwa na maendeleo yaliyo na mchango wa makundi yote kwenye jamii.

Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa akiongea katika kongamano hilo amesema, Ofisi ya Taifa ya Takwimu itahakikisha wanachukua taarifa sahihi kwa watu wenye ulemavu itakayosaidia serikali kutambua idadi na mahitaji yao ili waweze kuhudumiwa.

Awali, Mwenyekiti shirikisho la vyama vya Watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Ernest Kimaya alisema lengo la kongamano hilo ni kutoa elimu kwa watu wenye ulemavu ili kuwa na uelewa ikiwemo kujua umuhimu wa sensa ya watu na makazi.

Amesema sensa ya watu na makazi kwa Watu wenye Ulemavu kwa Bara na Visiwani ili ifanikiwe inahitaji ushirikiano hivyo kuwahimiza Watanzania wote kuhakikisha wanasimamia maagizo ya Serikali na kuhimizana ushiriki wa jambo hilo muhimu kwa Taifa.

Kibu Denis kutetea tuzo Simba SC, Mashabiki wapewa shukurani
Seattle Sounders kumuunga mkono Rais Samia kuinua Sanaa, Michezo