Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi, zitawasaidia wafanyabiashara kutathmini uwezo wao kibiashara na mitaji, ili kutoa faida na kutafuta maeneo mapya ya uwekezaji.

“Wafanyabishara wakubwa kwa wadogo hutumia takwimu za sensa kutathmini uwezo wa kibiashara wa makampuni, uwezo wa mitaji kutoa faida na kutafuta maeneo mapya, ya uwekezaji na kupitia takwimu za sensa, menejimenti na bodi za makampuni ya biashara na taasisi za uwekezaji za ndani na nje, hupata uhakika wa kitakwimu ambao huwaongezea kujiamini na kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati,” amesema.

Majaliwa, ameyasema hayo hii leo Jumatatu, Agosti 15, 2022, wakati akizungumza na wadau wa sekta binafsi juu ya umuhimu wa ushiriki wao, kwenye Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika nchini Agosti 23, 2022 kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Amesema, wafanyabiashara wanategemea takwimu za sensa kufanya maamuzi ya uwekezaji, ikiwemo huduma mbalimbali, upanuzi wa shughuli na maghala ya kuhifadhia na kusambazia bidhaa, maeneo bora ya kutangaza biashara, masoko mapya na kubuni bidhaa mpya pamoja na aina ya huduma za hospitali, sehemu za starehe na sehemu za kufanyia mazoezi.

“Sensa ya Watu na Makazi ni muhimu kwa kuwa moja ya mikakati ya kiuchumi ya Tanzania ni kuvutia uwekezaji na kuboresha kiwango cha maisha cha wananchi wake. Uwepo wa takwimu bora za Sensa ya Watu na Makazi utasaidia kuharakisha utekelezaji wa mikakati hiyo,” amesema Waziri Mkuu.

Aidha, Majaliwa pia ametoa pongezi kwa vyombo vya Habari kwa ushiriki wao katika kutoa hamasa kwa jamii, na kuwaelezea umuhimu wa sensa ikiwemo kuwajulisha siku ya kuhesabiwa, na kudai kuwa utafiti uliofanywa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), Julai mwaka huu ulionesha kuwa asilimia 98 ya Watanzania wanatambua uwepo wa sensa.

“Kitendo cha kuwaonesha wananchi nini kitaulizwa, kimesaidia kuwaandaa wananchi kuhusu zoezi hili. Wasanii mbalimbali nchini wametoa elimu kwa kiwango kikubwa, viongozi wa dini nao wamefanya kazi kubwa na nzuri sana ya kuwaandaa wananchi, ninawashukuru sana.”

Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wadau hao, Waziri wa Nchi (OWM-SBU), George Simbachawene amesema maandalizi ya zoezi la sensa yamefikia asilimia 95 na kwamba asilimia tano iliyobakia watajitahidi ili tufike kwenye ufanisi unaotarajiwa wa asilimia 100.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Paul Makanza amesema wameshirikiana na Serikali katika vikao kadhaa na kuainisha maeneo saba ambayo wanaweza kuunga mkono.

Ameyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni utoaji wa huduma, vifaa, utoaji elimu, usafiri, usafirishaji wa vifaa, utoaji wa matangazo na kuchangia mafuta ya magari. Alisema baadhi ya kampuni za simu zilianza kurusha jumbe fupifupi kwa wateja wao, vituo vya redio na televisheni navyo vilianza matangazo kuhamasisha jamii.

Matokeo Kenya: Ngumi zarushwa ukumbi wa matangazo, Tume yagawanyika.
Kenya: Wagombea walivyowasili Bomas tayari kwa matokeo