Mshambuliaji wa zamani wa Young Africans, Amissi Tambwe amesema bado hajalipwa fedha anazoidai klabu hiyo, licha ya siku 45 walizopewa na Shirikisho la Soka la Duniani ‘FIFA’ kumalizika.

Tambwe amesema mpaka sasa hajui chochote juu ya malipo ya fedha zake kutoka Young Africans, licha ya kuwapa hesabu zote kwani hata wakili wake, Felix Majani hajui lolote kutoka ndani ya klabu hiyo.

Tambwe ametoa kauli hiyo baada ya kuona kimya kimetawala kutoka kwa viongozi wa Young Africans, ambao walijinasibu kuwa tayari kumlipa kufuatia sakata la madai yake kupamba moto majuma mawili yaliopita.

“Binafsi hakuna ambacho kwa sasa najua kutoka Yanga zaidi ya kwamba bado hawajanilipa licha ya kupigiwa simu na Injinia, Hersi Saidi na kuniambia nifanye mahesabu ya pesa ambazo nawadai, mwanasheria wangu amefanya hivyo, akawatumia lakini hakuna jambo lolote jipya.”

“Ninachojua kwamba Fifa waliwapa siku 45 wawe wameshalipa lakini hadi sasa zimeisha na hakuna lolote, hivyo hawezi kufanya usajili wowote katika usajili ujao hadi wawe wamelipa na kuwasiliana na mwanasheria wangu ili arudishe taarifa Fifa,” Amesema Tambwe.

Mshambuliaji huyo kutoka nchini Burundi anaidai Young Africans kiasi cha Shilingi milioni 45 ambazo alipaswa kulipwa akiwa ndani ya klabu hiyo, lakini hadi anaondoka miaka miwili iliopita alikua hajalipwa.

TFF yatangaza vituo Ligi ya Mabingwa 'RCL'
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Februari 24, 2021