Mwenyekiti Halmashauri Kuu Taifa, Sheikh Hamisi Mataka amesema kwa niaba ya Mufti wa Tanzania na Sheikh mkuu, tukio la mtumishi wa Serikali kuchana quran tukufu linalaaniwa vikali huku akilipongeza jeshi la Polisi kwa hatua walizochukua.

Amesema kitendo cha kuchana ni kitendo kibaya chenye kuvuta hisia na kinachoweza kusababisha uvunjifu wa amani, lakini amewaomba Waislamu watulie na kuacha sheria ifuate mkondo wake.

“Kwakua tayari amekamatwa na sheria inachukua mkondo wake niwaombe waislamu watulie na kuiachia mahakama kufuata taratibu zake, pia tusitumie mitandao ya kijamii kulisambaza tukio hili kwa nia ya kuchochea kwani tayari muhusika amekamatwa na anapelekwa mahakamani” Amesema Sheikh Mataka.

Awali amesimulia kwa ufupi tukio hilo lilivyo tokea na amewapongeza sana Waislamu wa Kilosa kwa kutochukua sheria mkononi na zaidi kuchukua hatua ya kuviarifu vyombo vya usalama.

“Alifika katika eneo la msikiti ambalo linauza vitabu vya dini vya kiislamu akanunua juzuu za quran tatu na akaenda katika eneo la baa moja na akaanza kuchana quran, anaitemea mate, akainajisi na baadae akochoma moto” ameeleza Sheikh Mataka

Aidha ametoa wito kwa waislamu wote tukio lolote linapotokea kutohamaki na kugathibika na kuchukua sharia mkononi.

“Nasaha yetu kwa dini zote hapa nchini tuzingatie misingi ya kuishi kwa pamoja kwa amani, na msingi mkuu ni kuheshimu matukufu ya mwenzako, pamoja nakuvumiliana” amesisitiza Sheikh Mataka

WHO yatangaza Dunia inakabiliwa na uhaba vifaa vya kujikinga na Corona
Aliyechana Quran atiwa mbaroni, Waziri Jafo aingilia kati