Meneja wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zakayo Temu ameomba mkoa huo kupewa hadhi ya mkoa maalum ili uweze kukabiliana na changamoto za ujio wa Serikali Dodoma.

Mhandisi Temu ametoa ombi hilo, Oktoba 2, 2016 wakati akitoa taarifa ya utendaji wa TANESCO Mkoa wa Dodoma mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alifika kwenye kituo cha kupozea umeme cha Zuzu nje kidogo ya mji wa Dodoma, kukagua mahitaji halisi ya umeme ikilinganishwa na ujio wa watumishi mkoani humo.

Amesema kuwa TANESCO inaomba mkoa wa Dodoma ambao ni Makao Makuu uangaliwe kwa jicho la pekee na kupewa hadhi ya mkoa maalum kama ilivyo kwa Dar es Salaam ambako kuna mikoa minne ya ki-TANESCO ambayo ni ya Ilala, Kinondoni, Temeke na Mikocheni.

Amesema Dodoma inatakiwa kubeba majukumu yote ya Serikali kama yanavyofanyika hivi sasa katika Jiji la Dar es Salaam. Hivyo, wanaomba tupewe kipaumbele kwenye rasilmali watu, usafiri na vitendea kazi ili kuiwezesha TANESCO iende kwa kasi zaidi na kumudu wimbi la wafanyakazi wanaohamia Dodoma.

Mhandisi Temu amesema kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 400 kutoka Iringa mpaka Shinyanga kupitia Dodoma, kumeboresha upatikanaji wa umeme kwenye mji wa Dodoma.

Amesema kazi inayoendelea hivi sasa ni kubadilisha nguzo za umeme zilizochakaa; kubadilisha njia za msongo wa kilovolti 11 kwenda kilovolti 33 zenye urefu wa km. 85 na transforma 74 ili kupunguza upotevu wa umeme na kuingiza njia hizo kwenye njia mpya ya 132/33kV katika maeneo ya manispaa ambayo yanapata umeme kupitia njia za 11kV.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza viongozi wa TANESCO mkoa wa Dodoma wahakikishe wanapeleka miundombinu ya umeme kwenye maeneo yanayopimwa viwanja ili wanaonunua wakute huduma hiyo ipo tayari.

“Nimeongea na watu wa idara ya maji, nimewaambia wapeleke miundombinu yao katika maeneo yanayopimwa viwanja. Na ninyi pia mfanye hivyo kama ambavyo watu wa TAMISEMI walijenga barabara za lami katika viwanja vipya vya makazi ili watu wakienda kununua wakute huduma hiyo ipo tayari,” alisema.

Majaliwa amesema amefarijika kukuta Dodoma hatuna shida ya umeme, hatuna mgao, kwa hiyo amewataka TANESCO k endeleza kazi hiyo nzuri wanayoifanya.

Waziri Mkuu aridhishwa na maeneo yaliyotengwa kujenga miundombinu Dodoma
JPM amteua Prof. Lawrence Museru kuwa Mkurugenzi Mtendaji Muhimbili