Waziri wa Madini, Dkt. Dotto Biteko ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa kinu cha kupoza umeme (substation) kinachojengwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), utakaosaidia kuachana na uzalishaji wa umeme wa mafuta na kuhamia umeme wa Gridi ya Taifa, huku Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), likitarajia kupata shilingi bilioni tano za kitanzania kwa mwezi, za mauzo ya umeme.

Biteko ameyasema hayo, katika ziara yake aliyoifanya katika Mgodi wa GGML uliopo Geita, ambapo hadi kufikia Machi 2023, GGML itaanza kutumia umeme wa gridi ya Taifa na kuongeza kuwa, “GGML wanataka kuhama kutoka kwenye matumizi ya umeme unaozalishwa kwa mafuta kwenda kwenye umeme wa TANESCO, kupitia substation inayojengwa kwa dola za Kimarekani milioni 20”.

Awali, Makamu Rais wa kampuni ya AngloGoldAshanti inayomiliki Geita Gold Mining Limited (GGML), Simon Shayo amesema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza gharama za uendeshaji wa mgodi na uzalishaji wa umeme kwa asilimia zaidi ya 50.

Mgodi wa GGML unatumia zaidi ya MW 40 zinazozalishwa kwa kutumia jenereta zinazotumia mafuta ya dizeli tangu mwaka 2018, na Shayo amesema, “Sasa tupo kwenye mchakato wa kujenga kinu cha kupoozea umeme chenye thamani ya karibu Shilingi za Kitanzania bilioni 50 na TANESCO watajenga njia ya kilomita sita kufikia hapa.

“Kwa hiyo hadi kufikia Machi mwaka 2023, tutakuwa tumeingia kwenye umeme wa TANESCO, na tutakuwa tumepunguza gharama yetu ya umeme kufikia asilimia 50, kutoka uniti moja kwa senti 19 kwenda kwenye unit moja kwa senti tisa (US $),” alisema Shayo.

Mgodi huo wa GGML, unajenga kinu hicho kitakachokuwa na uwezo wa kupitisha umeme wenye kilovolt 13 kwenye mitambo yake ambapo hadi kikamilike kinatarajiwa kugharimu kiasi cha Sh. bilioni 50, huku Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), nalo likijenga njia ya kupeleka umeme katika mgodi wa GGML yenye urefu wa kilomita sita.

Wito kuungana na ‘mama’ kutangaza vivutio vya Utalii
Ally Kamwe aichimba mkwara Simba SC