Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umewataka wananchi kutotupa taka hovyo na kutofanya biashara katika maeneo yaliyotengwa kwa shughuli mbalimbali ikiwemo waenda kwa miguu, ili kuepusha usumbufu na madhara yanayoweza kujitokea.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo TANROADS mkoa wa Dar es Salaam, Eliseus Mtenga wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ziara ya ukaguzi wa matumizi ya fedha za kukarabati barabara zilizotolewa na Mfuko wa Barabara Tanzania.

Mtenga amesema kuwa kwa sasa kumekuwa na wafanyabiashaara hasa machinga wanaotumia eneo la waenda kwa miguu, na hivyo kuwalazimu wanaotembea kwa miguu kupita pembezoni mwa barabara kuu, hali inayoweza kusababisha ajali na kupelekea majeraha, ulemavu au kifo.

Aidha, amewaonya wale wote wanaotupa takataka kwenye mitaro ya maji taka kuacha mara moja kwani kuziba kwa mitaro hiyo kutasababisha mafuriko yanayohatarisha usalama wa raia, mali zao na miundombinu ya barabara.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Joseph Haule ameiagiza TANROADS kufuatilia, kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote waliounganisha mifumo yao ya maji taka kwenye mitaro ya barabarani vitendo ambavyo vinaweza kuababisha magonjwa mbalimbali kama vile kipindupindu.

Rais Samia: Wanamichezo mkapate chanjo ya Corona
Prof. Mkumbo: TANTRADE itoe taarifa, takwimu sahihi