Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) imesema kuwa itaendelea kuimarisha mitandao ya wadau na makampuni mbalimbali ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo nchini wanapatiwa fursa za masoko ili kuweza kukuza sekta ya biashara nchini.

Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE Zanzibar, Latifa Khamis wakati wa mkutano wa ana kwa ana baina ya wafanyabiashara, wazalishaji na wanunuzi wa bidhaa za ngozi na shule katika Maonyesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF).

Amesema kuwa Serikali kupitia TANTRADE itaendelea kutumia majukwaa na fursa mbalimbali za kibiashara kwa ajili ya kuwawezesha wajasirimali na wafanyabiashara kuweza kutumia fursa zilizopo ikiwemo kupata masoko ya uhakika ya biashara zao kupitia kwa wadau mbalimbali waliopo ndani na nje ya nchi.

“TANTRADE imeandaa mkutano huu maalum kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo kuweza kupata fursa za masoko ya kuuzia masoko yao ambapo utaratibu huu utakuwa endelevu, hivyo kampuni ya  DHL kupitia Market Plaze Africa wametoa fursa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa hapa nchini kutangaza biashara zao,”amesema Latifa.

Aidha, amesema kuwa mara baada ya kuisha kwa maonyesho ya 43 ya DITF, TANTRADE imeandaa mkakati maalum wa kuwaunganisha wajasiriamali wadogo na wafanyabiashara kupitia maonyesho ya bidhaa za wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo nchi nzima ambapo wataanzia katika Mkoa wa Ruvuma na baadae Zanzibar.

Kwa upande wake Meneja Mkazi wa Kampuni ya DHL Tanzania, Paul Makolosi amewataka wajasirimali na wafanyabiashara wadogo kutangaza bidhaa zao katika taasisi hiyo kwa kuwa masoko ya bidhaa zao yapo kwani nchi nyingi za mabara ya Ulaya na Amerika yamekuwa wakivutiwa na bidhaa zinazozalishwa katika nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania.

JPM aagiza familia ya Mujungi ijengewe nyumba ya kisasa
Kamanda Mambosasa aelezea ‘mashaka’ kutekwa kwa msaidizi wa Membe