Kumeanza kuzuka minong’ono mbalimbali nchini kuhusu uwakilishi wa Tanzania mwakani kwenye michuano ya klabu inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na hii ni mara baada ya Yanga kufuzu kwa hatua ya makundi ya michuano Kombe la Shirikisho Afrika jana.

Yanga imefuzu hatua hiyo mara baada ya kuitupa nje Sagrada Esperanca ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, ikipigwa ugenini 1-0 lakini ushindi wa 2-0 walioupata nyumbani uliwabeba Wanajangwani hao.

Minong’ono iliyoanza kuzuka ni kuwa, Simba itapanda ndege mwakani kupitia mgongo wa Yanga wa kufika hatua hiyo kwenye michuano ya CAF.

Lakini minong’ono hii ni sawa na ndoto za alinacha kutokana na kanuni za michuano hiyo kuibana Tanzania na nchi zote za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) isipokuwa Sudan tu, ambayo ndiyo imekuwa mkombozi wa ukanda huo kwa kuwa na rekodi ya kufanya vizuri.

Najua unataka kujua nini hicho hasa kinachoibana Tanzania na nchi za CECAFA kwa ujumla isipokuwa Sudan, jibu ni moja tu hakuna hata nchi moja iliyoweza kufikisha pointi 12 au kuendelea zinazohitajika ili Taifa fulani liweze kuongezewa timu kutoka moja hadi mbili katika kila michuano ya CAF ngazi ya vilabu.

Hiyo inatokana na timu za wawakilishi za ukanda huo kutokuwa na rekodi ya kufanya vizuri ndani ya michuano hiyo mara nyingi zikiishia raundi za awali ambazo hazina pointi, kwa mujibu wa viwango vipya vilivyotolewa na CAF kuanzia mwaka 2010 -2014 na vijavyo vya miaka mitano mingine ijayo vitatolewa 2018 na hivi vitaangalia zaidi matokeo.

Rekodi ya viwango hivyo vya CAF inaiumbua ukanda wa CECAFA kwani hakuna hata nchi moja ukiiondoa Sudan, iliyoweza kujinyakulia hata pointi moja kutokana na kufanya huko vibaya ndani ya michuano hiyo.

Sudan yenyewe imekuwa ikibebwa na timu kongwe za huko El Merreikh, Al Hilal, ambazo zimeifanya nchi hiyo kufikisha jumla ya pointi 33 wakiwa nafasi ya tano kwa mujibu wa viwango vya CAF na hiyo ni kutokana na kufanya vizuri kwa timu zake hizo.

Kwa Yanga kuingia hatua ya makundi (robo fainali) ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu, sasa kunaihakikishia Tanzania kuandika pointi moja na sasa ikidaiwa pointi nyingine 11 ili iweze kuongezewa timu moja moja katika kila michuano hiyo mikubwa ya klabu barani Afrika.

Yanga ikiingia hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo basi itakuwa na uhakika wa kuifanya Tanzania kuwa na alama mbili na ikifika fainali basi nchi hiyo itajikusanyia pointi tatu kama timu hiyo itapoteza fainali na pointi nne kama Wanajangwani hao wakiibuka mabingwa.

Kwa Afrika ni nchi 12 pekee ambazo zimejihakikishia nafasi ya kuingiza timu mbili mbili katika kila michuano hiyo CAF, Tunisia ikiwa kinara, ikifuatiwa na Misri, Congo DR, Algeria, Sudan, Ivory Coast, Morocco, Cameroon, Congo Brazzaville, Mali, Nigeria na Afrika Kusini, iliyoanza kufanya vizuri kwa miaka ya hivi karibuni.

Ni mtihani mkubwa sana kwa Tanzania na nchi za CECAFA inaotakiwa kuhakikisha inaufanya ili nchi wanachama ziweze kuongezewa uwakilishi katika michuano hiyo na ni lazima zisafe sana kuweza kufikia mafanikio waliyofikia timu hizo 12.

Kwani ili ujihakikishie ubora wewe mwenyewe na nchi yako kufika huko ni lazima uweze kupambana vilivyo na mataifa hayo 12 yanayoongoza kwa ubora katika ngazi ya klabu barani Afrika, la sivyo kila mwaka tutaishia kupeleka timu moja moja.

Kimahesabu ndani ya miaka miwili ijayo kwa upande wa Tanzania, ili tuweze kupeleka timu mbili mbili katika kila michuano ni lazima Yanga mwaka huu ihakikishe inaingia fainali na kuchukua kombe la michuano hiyo ili iihakikishie nchi pointi nne.

Na pia mwakani Yanga (Ligi ya Mabingwa) na Azam FC (Kombe la Shirikisho) zitakazoliwakilisha Taifa katika michuano hiyo zihakikishe zinachukua makombe ya michuano hiyo. Hii itaifanya Tanzania kupeleka timu mbili mbili (nne) mwaka 2018 katika michuano hiyo.

Imeandaliwa na ABDUCADO EMMANUEL.

La Liga Kuzibana Vikali Klabu Za Nchini Hispania Kuanzia 2016-17
Hivi Punde: Ndege yapotea angani ikiwa na abiria 66