Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Serikali imejiwekea mkakati wa kuhakikisha Tanzania inapata chanjo chanjo kwa asilimia 60 ili kuhakikisha inapambana na ugonjwa wa Uviko-19.

Msigwa ameyasema hayo leo Agosti 1, 2021 kwenye mkutano na wanahabari ambapo amesisitiza kuwa chanjo bado ni hiari na kesho Agosti 2, 2021 zitaanza kutolewa nchi nzima kwenye zaidi ya vituo 550.

”Rais Samia Suluhu anafanya kazi kubwa sana kuhakikisha Tanzania inapata chanjo nyingi iwezekanavyo, kwasababu nchi yetu imejiwekea tupate asilimia kama 60 hivi ambapo tutakuwa tumejihakikishia kukata maambuzi ya ugonjwa huu wa Uviko-19” amesema Msigwa

”Nchi zote zitasaidiwa chanjo kwa idadi ya asilimia 20 ya watu wake, kwahiyo Tanzania kupitia mpango huu tutapata takribani chanjo milioni 11, kwahiyo zilizokuja hizi zaidi ya milioni 1 ni sehemu ya mpango wa COVAX Facility chini ya WHO” amesema Msigwa

Pia ameongeza kuwa ”Zoezi la chanjo litaanza kutolewa kesho kuna vituo kama 550 vilivyoandaliwa, chanjo hazijaleta madhara kwa waliotumia kama tulivyokuwa tunasikia. Chanjo zitaendelea kuletwa baada ya zile dozi milioni 1 kuna nyingine zitaendelea kuletwa”

”Tungependa wananchi kwenye suala hili la chanjo wajitajidi sana kuwasikiliza wataalam wetu wanasemaje, maana hivi sasa kila mtu amejivisha utaalam anaijua Corona lakini serikali imetoa muongozo na ni vyema watu wausome na kuufuata”

“Msimamo wa Serikali ni kwamba shughuli ziendelee kama kawaida lakini Watu wachukue tahadhari, Wizara ya Afya imeandaa Mdahalo kesho pale Muhimbili wale wote wenye hoja waende wakatoe hoja zao watajibiwa, hoja inajibiwa kwa hoja” amesema Msigwa

Mayele atambulishwa Young Africans
Rais Samia kuanza ziara ya siku mbili nchini Rwanda