Tanzania imeahidi kushirikiana na Jumuiya ya Madola kukabiliana na changamoto za kidunia zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, Uviko – 19, migogoro, ugaidi na umasikini.

Ahadi hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi. Samwel Shelukindo katika maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.

Amesema licha ya uhusiano wetu na historia ya pamoja kama wanachama wa Jumuiya ya Madola tunaamini kuwa kwa umoja wetu tunaweza kuzikabili changamoto za kidunia kwa urahisi zaidi.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo akiwasilisha hotuba yake katika maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.

“Kila mmoja wetu akitimiza wajibu wake kwa wakati, itakuwa rahisi kuzikabili changamoto za kidunia hususan mabadiliko ya tabianchi, Uviko 19, migogoro, ugaidi na umasikini,” ameongeza Shelukindo.

Kwa Upande wake, Balozi wa Uingereza hapa Nchini, David Concar amesema Jumuiya ya Madola imekuwa na mchango mkubwa kwa Tanzania hususan vijana ambao ndiyo taifa la kesho wamekuwa wakinufaika na ufadhili wa masomo kwa ngazi mbalimbali, biashara na uwekezaji pamoja na ajira.

Amesema Jumuiya ya Madola imefurahishwa na hatua ambazo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikizichukua katika masuala ya demokrasia, haki za binadamu na utawala bora, ulinzi na usalama na utawala wa sheria.

Balozi wa Uingereza hapa Nchini, David Concar akichangia jambo wakati wa maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.

“Tanzania imeboresha sana masuala ya demokrasia, haki za binadamu na utawala bora, ulinzi na usalama na utawala wa sheria….. mtakumbuka hivi karibuni mikutano ya kisiasa imeruhusiwa pamoja na uhuru wa vyombo vya Habari umeongezwa jambo ambalo linaashiria kukua na kukomaa kwa demokrasia,” alisema Concar.

Maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Madola, yamehudhuriwa pia na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba pamoja na baadhi ya wanamichezo wa Tanzania walioshiriki kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola yakiwa na Kauli Mbiu isemayo ‘Kujenga mustakabali endelevu na wenye amani wa pamoja.

Makamu wa Rais ataka ubunifu utatuzi wa migogoro
Kocha Tanzania Prisons awatuliza mashabiki