Tanzania na Qatar zimefanya mazungumzo na kuweka mikakati mbalimbali ikiwemo utayari wa vijana wa Tanzania kufanya kazi nchini humo, hasa katika kipindi hiki cha mahitaji ya nguvukazi kutokana na uwenyeji wa Mashindano ya Mpira wa Miguu wa Kombe la Dunia yatakayochezwa mwezi Novemba 2022.

Mazungumzo hayo yamefanyika baina ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Dkt. Ahmad Hassan Al-Hamadi kwenye Ofisi za Wizara hiyo Jijini Doha, Qatar Agosti 28, 2022.

“Tunawapongeza Qatar kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia, Tanzania imewaandaa vijana wake wenye ujuzi tunaomba kupata nafasi za ajira na za viza kwa ajili ya Watanzania kuweza kuja kufanya kazi huku hasa wakati huu wa kombe la dunia,” amesema Balozi Fatma.

Katika Kikao hicho, viongozi hao pia wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo mbili katika maeneo ya uwekezaji na biashara, ambapo Balozi Fatma amesema Serikali imefanya maboresho ya mazingira ya uwekezaji na biashara.

Amesema, kupitia maboresho hayo, wafanyabiashara wa Qatar wanakaribishwa kuwekeza nchini Tanzania katika maeneo mbalimbali kama vile utalii, kilimo, madini, maliasili, uvuvi na utamaduni.

Mkutano huo ulioandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, pia umehudhuriwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza na Mkuu wa Utawala wa Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar, Bi Patricia Kiswaga.

Tanzania yawasilisha miradi nane TICAD 8
PSPTB:Wanunuzi wa Umma wasiojisajili watasaga meno