Serikali ya Tanzania na Serikali ya Poland zimekubaliana kuongeza ushirikiano katika biashara, na kuwataka wafanyabiashara kutoka nchi zote mbili kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara.

Makubaliano hayo yalifanyika Jijini Dar es Salaam jana (Septemba 20, 2019) ambapo serikali ya Tanzania iliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi ili hali Poland iliwakilishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Marcin Przydacz.

Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya makubaliano hayo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi amesema kuwa lengo la makubaliano hayo ni kukuza ushirikiano uliopo kati ya nchi hizi.

“Kwa sasa, tunashirikiana na Poland katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na biashara ambayo takwimu zinaonesha kwamba biashara kati ya Tanzania na Poland zimepanda kutoka milioni 77.7 mwaka 2016 mpaka milioni 124.5 mwaka 2017. Bidhaa za Tanzania zinazouzwa Poland ni pamoja na chai, kahawa na tumbaku. Tanzania inanunua Poland bidhaa mbalimbali kama tairi za magari, vifaa vya maabara na vifaa vya umeme,” alisema Prof. Kabudi

Prof. Kabudi aliongeza kuwa, fursa za biashara baina ya nchi hizi mbili bado ni nyingi na imekubaliwa kuwa balozi zetu na taasisi zingine za Serikali zetu zitumike kuongeza ushirikiano katika biashara. “Kwa hili, tunawaomba wafanyabishara wetu kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara,” Aliongeza Prof. Kabudi

Kwa mujibu wa Waziri Kabudi, Tanzania na Poland zinashirikiana kwenye miradi mikubwa miwili. Mradi wa kwanza ni wa kiwanda cha kuunganisha trekta, kilichopo Kibaha ambao unatekelezwa kwa mkopo wa riba nafuu kutoka Serikali ya Poland. Kupitia mradi huu, jumla ya trekta 2400 zinaunganishwa nchini kupitia kampuni ya URSUS ya Poland. Tayari trekta 875 zimeshaunganishwa. Mradi huu utaongeza uzalishaji kwenye sekta ya kilimo na kuleta mapinduzi ya kilimo kutoka kutumia jembe la mkono kwenda kutumia trekta.

Mradi mwingine ni ule wa kujenga maghala ya kuhifadhia nafaka ambapo jumla ya maghala 8 yanajengwa katika kanda zote zinazohifadhi chakula nchini. Mradi huu utaongeza uwezo wa Serikali wa kuhifadhi nafaka kutoka tani 250,000 kwa sasa hadi tani 500,000.

Katika hatua nyingine, tumekubaliana pia kutoa fursa ya elimu ambapo watanzania sasa watapata fursa ya kwenda kusomaPoland ambapo fursa nyingi zitatolewa katika fani ya udaktari wa aina mbalimbali, uhandisi, sayansi, Tehama, kilimo na maeneo mengine.

Prof. Kabudi aliongeza kuwa, Tanzania imeendelea kuvutia watalii kutoka nchi ya Poland. Kila mwaka, watalii wapatao 12,000 wamekuwa wakitembelea visiwa vya Zanzibar kwa ndege zinazotoka miji mbalimbali ya Poland moja kwa moja mpaka Zanzibar. Idadi ya watalii inaendelea kuongezeka kutoka watalii 12,241 mwaka 2017 hadi watalii 18, 853 mwaka 2018.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Marcin Przydacz amesema kuwa Serikali yake itaendelea kuwahimiza Wapoland kuja kuwekeza nchini kwa wingi na hasa kwenye maeneo ya uzalishaji wa dawa, kilimo hususan katika uongezaji wa thamani ya mazao ya kilimo, uzalishaji wa mashine za viwandani na uzalishaji wa bidhaa za viwandani.

Pia, Waziri Przydacz ameahidi kuwa Serikali yake itaendeleea kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano inayooongozwa na Mhe. Rais Magufuli ya kutafuta suluhisho la changamoto ya uhaba wa maji inayokabili wananchi sehemu mbalimbali nchini.

Uteuzi wa JPM wawaibua wasomi, wanasiasa, Fatma Karume asimamishwa uwakili
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Septemba 21, 2019