Maafande wa Jeshi la Magereza ‘Tanzania Prisons’ wameapa kuvunja rekodi ya Young Africans ambao hawajafungwa tangu Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21 ulipoanza mwezi Septemba.

Keshokutwa Alhamis (Desemba 31), Tanzania Prisons yenye alama 21 ikiwa nafasi ya 11, itakua wenyeji wa Young Africans inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa alama 43, kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Katibu mkuu wa Tanzania Prisons Ajabu Kifukwe amesema mbali na kupanga kuvunja rekodi ya Young Africans, pia watautumia mchezo huo kulipa kisasi cha kuharibiwa rekodi yao ya kutopoteza mchezo hata moja kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, na sasa amedai kuwa ni zamu yao.

Amesema anaamini kuwa mchezo wa kesho kutwa hautokuwa rahisi, lakini na wao pia ni timu nzuri na wamejipanga kukabiliana na Young Africans ambayo imemaliza mzunguko wa kwanza bila kupoteza mchezo hata moja, ikicheza michezo 17, ikishinda 13 na kutoka sare nne na ndiyo inayoongoza kwenye msimamo wa ligi mpaka sasa.

“Young Afrcans haijapoteza mechi, sisi tumejipanga kuwa timu ya kwanza kuifunga na kuharibu rekodi hiyo kama walivyotufanyia wao msimu uliopita,” amesema Ajabu Kifukwe.

Msimu uliopita, Prisons ilikuwa timu pekee kwenye Ligi Kuu ambayo ilicheza michezo 12 bila kupoteza, kabla ya kufungwa bao moja kwa sifuri dhidi ya Young Africans. Baada ya kushinda michezo minne na kutoka sare minane, Tanzania Prisons ilichapwa bao moja kwa sifuri kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa Desemba 27, mwaka jana kwa bao la Mnyarwanda, Patrick Sibomana.

Wananchi 662 kunufaika na Bima ya afya
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Desemba 29, 2020