Baada ya kuambulia kisago cha Mabao 7-1 mwishoni mwa mwaka 2022, Benchi la Ufundi la Maafande wa Jeshi la Magereza ‘Tanzania Prisons’ limesisitiza halitarudia makosa kwenye mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Tanzania Prisons itakua Mgeni wa Azam FC katika Uwanja wa Azam Complex-Chamazi jijini Dar es salaam Jumatatu (Januari 16).

Kocha Msadizi wa Maafande hao kutoka jijini Mbeya Shaban Mtupa amesema, maandalizi ya kikosi chao yapo vizuri kuelekea mchezo huo ambao watacheza katika Uwanja wa ugenini.

Mtupa amesema hakuna ugumu wowote uliopo mbele yao kwa sasa, cha muhimu wamejipanga vizuri kwenye safu zote hususan ile la Ulinzi na Ushambuliaji.

Amesema wamekua na muda wa majuma mawili ambao wameutumia kurekebisha makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo dhidi ya Simba SC, ambapo ilishuhudiwa wakipokea kichapo kikali cha 7-1.

“Tumepata muda wa kufanya maandalizi vizuri, kila mchezaji ameshafahamu wapi tulipokosea tulipocheza dhidi ya Simba SC, hivyo tunakwenda kwenye mchezo wetu na Azam FC tukiwa kamili.”

“Dhamira yetu ni kupata alama tatu, tunaamini hilo linawzekana kwa sababu tumejiimarisha katika safu zote hususan ile la Ulinzi na Ushambuliaji, ambazo zitakua na kazi ya kutupa matokeo chanya.”

Kwenye mchezo dhidi ya Azam FC, Tanzania Prisons itamkosa Mshambuliaji wake Samson Bangula anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyooneshwa wakati wa mchezo dhidi ya Simba SC kufuatia rafu mbaya aliyochezea Beki Enock Inonga Baka.

Robertinho avunja ukimya zawadi ya Kibu
Haikuwa rahisi Zanzibar 1964