Serikali ya Tanzania imeagiza wananchi kuhakikisha wanavaa barakoa wanapokuwa kwenye maeneo ya msongamano na kwamba wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa watapimwa katika kusimamia agizo hilo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa ingawa Kamati maalum iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan ilisema Tanzania iko salama, ilisema pia kuwa kuna tishio la wimbi la tatu la maambukizi ya virusi vya corona (covid-19) ambalo linazikumba nchi jirani zikiwemo Congo na Uganda.

Akizungumza Juni 12, 2021 Dkt. Dorothy aliwataka watanzania kurejesha utaratibu wa kuvaa barakoa, kunawa mikono na kutumia vitakasa mikono (sanitizer) kama hatua za kujikinga dhidi ya maambukizi ya covid-19.

Aidha, alisema Serikali itawatumia wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kufikisha elimu kwa wananchi kupitia kamati zao za afya ya msingi, kwakuwa baadhi ya wananchi hawajapata elimu.

“Kule waliko wana kamati zao zinazoitwa kamati za afya ya msingi, ambazo mwenyekiti wake ni mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya, wao wanatakiwa waite sekta zote zilizopo pale iwe ni elimu, kilimo, maji wajadili na kupeana kazi juu ya miongozo ambayo Wizara tumekuwa tukiitoa ili kufikisha elimu kwa wananchi,” alisema Dkt. Gwajima.

“Lazima tuwatumie viongozi hawa na kadiri tunavyoenda tutasainishana nao mikataba ili kuwapima kulingana na haya, mkoa gani unafanya vizuri, tunaita ‘score card’ ambaye hajafanya vizuri tunadili na mamlaka yake ya kuwajibika,” aliongeza.

Hivi karibuni Shirika la Fedha Duniani (IMF) ilisema iko tayari kuipatia Tanzania msaada wa dola za kimarekani milioni 574, ikiendelea kuzingatia masharti ya kupambana na covid-19, ikiwa ni pamoja na kutoa takwimu za maambukizi ya corona.  

Mahakama yaahirisha hukumu ya Mdude wa Chadema
‘Flash’ yasababisha mauaji ya mwanafunzi