Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Uganda zimetia saini hati za makubaliano ya kushirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, uhamiaji na magereza.

Tukio hilo limefanyika leo  Septemba 6, 2019 jijini Dar es salaam wakati wa kongamano la kwanza la biashara na uwekezaji ambapo Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni wameshuhudia utiwaji saini wa hati hizo.

Waliosaini hati hizo ni Waziri wa Mambo ya nje ya nchi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi wa Tanzania na Sam Kutesa wa Uganda

Aidha, moja ya malengo makubwa ya kongamano hilo ni kuunda jukwaa linalowezesha na kuruhusu sekta binafsi kutoka Tanzania na Uganda kushirikishana uzoefu, kuunda mitandao ya biashara, kubaini fursa na changamoto za biashara inayoendelea na uwekezaji, na kuonyesha bidhaa na huduma zao kwenye maonyesho.

Pia kuwaweka pamoja Wafanyabiashara kutoka Uganda na Tanzania, wachambuzi wa mambo, wachumi, wataalamu wa sheria, mashirika ya kimataifa, mashirika ya kitaifa, washirika wa maendeleo na Taasisi za habari.

Kongamano hilo linaratibiwa na TPSF ambapo kutakuwa na maonyesho ya biashara, ambapo linatarajiwa kufanyika kwa siku mbili hapa nchini kuanzia leo Septemba 6 na 7, 2019 katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere uliopo Jijini Dar es salaam.

Yanga yapinga Zahera kufungiwa mechi tatu
Rais Magufuli amlilia Mzee Mugabe