Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) zimeahidi kuimarisha ushirikiano kwa maslahi ya pande zote mbili.

Hayo yamesemwa kwenye mkutano kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) hapa nchini, Mhe. Manfredo Fanti, uliofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Balozi Sokoine ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania inaridhishwa na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya ambao umepelekea kuzaa matunda yenye manufaa kwa pande zote mbili. Aidha, ameahidi kuendelea kuimarisha uhusiano huo kwa maslahi ya pande zote.

Kwa upande wake, Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) hapa Nchini, Mhe. Manfredo Fanti amesema Umoja huo utaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Napenda kukuhakikishia kuwa Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana kwa ukaribu na Tanzania kwa ajili ya kuleta maendeleo ya wananchi wake,” amesema Balozi Fanti.

Katika tukio jingine, Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine pia amekutana kwa mazungumzo na Kaimu Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Xu Chen katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wawili walijadili masuala mbalimbali ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa uwili (Bilateral Cooperation).

Vanessa Mdee akanusha kupata mtoto
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Julai 20, 2021