Tanzania imefungua ofisi ndogo ya Ubalozi Hongkong nchini China ambayo itahudumia masuala ya kidiplomasia na kuongozwa na Balozi wa Heshima wa Tanzania Dkt, Annie Wu aliyeteuliwa Septemba 2 mwaka huu na Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga wakati alipohudhuria mkutano wa mahusiano ya China na Afrika,  FOCAC huko Beijing nchini China.

Ofisi hiyo mpya katika jiji la Hongkong, nchini China itasimamia masuala ya kibalozi na kuwasogezea karibu huduma hizo, tofauti na hapo awali ambapo huduma za kibalozi zilikuwa zikipatikana Beijing.

Hayo yamesemwa Jijini Hongkong nchini China na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mbelwa Kairuki, ambapo amesema ni fursa kwa watanzania na wachina kutumia ofisi ya Hongkong kupata huduma mbalimbali katika ofisi hiyo kwa urahisi.

Kwa upande wake Balozi wa Heshima wa Tanzania nchini China, Dkt. Annie Wu ameonyesha kufurahishwa kuaminiwa na Serikali ya Tanzania kwa majukumu hayo ya heshima aliyopewa na kuihakikishia serikali kuwa pamoja na mambo ya kidiplomasia, ataitangaza Tanzania kwa wawekezaji ili kuvutia uwekezaji zaidi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha uwekezaji Tanzania, Geoffrey Mwambe amesema kuwa kufunguliwa kwa Ubalozi huo kutasaidia kuongeza uwekezaji zaidi, Kwani wafanyabiashara wa China watatumia Ubalozi huo katika kufuatilia masuala ya uwekezaji.

Kwa mujibu wa kituo cha uwekezaji Tanzania, TIC-China, China inaendelea kuongoza duniani kwa kuweka mitaji mikubwa nchini Tanzania, kwa zaidi ya dola Bilioni 5.8,  kuanzia mwaka 1990 mpaka 2017, ambapo kuna jumla ya miradi 723, huku ikitoa ajira 87,126 kwa thamani ya dola Milioni 5 962.74, ikifuatiwa na Uingereza, yenye miradi 936 ya thamani ya dola Milioni 5,540.07, iliyozaa ajira 274,401, na Marekani ikiwa na miradi 244 ya thamani ya dola milion 4,721.15, iliyozalisha ajira 51,880.

Tawimu hizo za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zimebainisha kuwa China inaendelea kuwa nchi yenye lengo la kuwekeza zaidi katika maeneo mbalimbali hapa nchini, yakiwemo  kilimo, viwanda, utalii, Ujenzi, Teknolojia ya Mawasiliano na maeneo mengineyo.

Marekani yazishtukia China na Urusi kuhusu Afrika
Wizara ya Afya yatoa zawadi ya Krismasi kwa wazee