Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Tanzania imefanikiwa kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kwa asilimia 58 kutoka 130,000 mwaka 2003, hadi 54,000 mwaka 2021 kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI, (PEPFAR).

Majaliwa ameyasema hayo wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 20 ya mafanikio katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI yaliyowezeshwa na Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) iliyofanyika katika Hotel ya Serena Jijini Dar es Salaam.

Amesema, kupitia mfuko huo ambao umeleta mabadiliko makubwa katika katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi umesaidia kupunguza vifo kwa asilimia 76 kutoka 120,000 mwaka 2003 hadi 29,000 mwaka 2021.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Majaliwa ameongeza kuwa, Serikali ya Tanzania itaendelea kuunga mkono mpango huo katika kujenga miundombinu ya afya, kutoa mafunzo, kutoa vifaa vya uchunguzi na vifaa vya kinga binafsi, na kuanzisha mifumo ya kufuatilia maambukizi.

“Serikali ya Tanzania inafahamu kwamba, Serikali ya Marekani ni mshirika mkubwa katika kukabiliana na Virusi vya Ukimwi nchini Tanzania, ikiwa imewekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni 6.6 kwa ajili ya kukabiliana na janga hiyo,” amesema Waziri Mkuu.

Amesema, PEPFAR kwa sasa unasaidia zaidi ya watu milioni 1.5 wanaoishi na VVU (WAVIU) kwenye matibabu kupitia mpango wa kuokoa maisha wa ARVs ambapo kabla ya kuanzishwa kwa mpango huo WAVIU wasiozidi 1,000 ndio walikuwa kwenye Tiba ya Kupambana na Virusi vya Ukimwi.

Aliyekuwa mke wa Manara aeleza uhusiano wake na Harmonize
SJMT na SMZ zinashirikiana kiuchumi: Waziri