Muigizaji mashuhuri wa filamu za Tanzania “Bongo movie” Mohamed Fungafunga maarufu kwa jina la Mzee Jengua amefariki dunia asubuhi ya leo Wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa chama cha waigizaji wa Bongo movie, Eliya Mjatta, marehemu Jengua amekutwa na umauti akiwa nyumbani kwa mtoto wake.

Msanii wa Bongo movie Blandina Chagula maarufu ‘Johari’, amethibitisha kufariki kwa msanii huyo na kueleza kwamba alikuwa akiugua kwa muda mrefu baada ya kupooza na kwamba alikuwa akiendelea na matibabu nyumbani kwa mwanaye, Mkuranga.

Mzee Jengua alipata umaarufu mkubwa katika mchezo wa runinga wa Kidedea uliokuwa ukirushwa na kituo cha ITV na kutayarishwa na Chemchem Arts Group, akiigiza kama mzee katili na mwenye roho mbaya.

Jengua aliigiza kwenye filamu za Kidedea, Handsome wa Kijiji, Kashinde na zingine nyingi.

Buriani Mohamed Fungafunga.

Koeman: Tunawaheshimu PSG, hatuwaogopi
Uongozi Mwadui FC wakanusha tuhuma