Msanii wa Muziki wa Dansi kutoka Jamhuri ya Watu wa Kongo, aliyewahi kuongoza Bendi ya ‘FM Academia, Wajelajela Orijino’ amefariki leo asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa.

Taarifa zilizotolewa na mwanamuziki mwenzake, Kardinal Gento aliyekuwa akimuuguza, zimeeleza kuwa Ndanda alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa vidonda vya tumbo na kwamba alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kuzidiwa alipokuwa katika Hospitali ya Mwananyamala.

“Nimekesha naye, ilipofika asubuhi hali yake ilikuwa nafuu, nikaondoka kurudi nyumbani kwa ajili ya chakula, nikaacha anafanyiwa mpango wa damu maana alikuwa amepungukiwa damu, lakini muda mfupi baada ya kuondoka hospitali hapo nikapigiwa simu kuwa Ndanda amefariki,” alisema Gento.

Mwanamuziki huyo alifariki majira ya saa mbili asubuhi katika hospitali hiyo.

Gonta ambaye ni mjomba wa Marehemu aliongeza kuwa bado mipango ya mazishi haijafahamika kwani mama yake Ndanda alikuwa anaelekea Lubumbashi nchini Kongo lakini amelazika kurejea Dar es Salaam. Hivyo, familia itaamua sehemu ya kumzika mwanamuziki huyo na kutoa taarifa kupitia vyombo vya habari.

Dar24 imeguswa na msiba huo na inatoa pole kwa ndugu jamaa na wadau wa muziki nchini.

Apumzike kwa Amani, Amina!

 

Ridhiwani 'anawa mikono' sakata la ufisadi wa Mabilioni ya Jeshi la Polisi
Aliyemuua Osama Bin Laden akamatwa