Kamati ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) imemteua Makamu Mwenyekiti wa TASWA, ambaye pia Mhadhiri Msaidizi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Egbert Mkoko kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo za Wanamichezo Bora Tanzania mwaka 2015/2016.

Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando pia amesema wameteua wajumbe tisa wa kamati hiyo, ambao ni pamoja na Mahmoud Zubeiry (Bin Zubeiry Sports), Jane John wa TBC, Baruani Muhuza wa Azam TV, Limonga Justine wa Redio Uhuru, Maulid Kitenge wa E-FM Redio, Deogratias Rweyunga wa Redio One na ITV), Shaffih Dauda wa Radio Clouds na TV, Asha Muhaji wa Bingwa na Nelly Mtema Daily News.

Kamati inaweza kuongeza wajumbe wengine au kupunguza kwa kadri itakavyoona inafaa. Utaratibu wa kuizindua kamati hiyo unaandaliwa na sekreterieti ya TASWA.

Jukumu la kamati itakuwa ni kuandaa utaratibu wa kuwapata wanamichezo watakaowania tuzo hiyo na pia kuteua washindi kwa kila mchezo.

Tuzo za Wanamichezo Bora zinazotolewa kila mwaka na TASWA zimepangwa kufanyika Agosti 26, mwaka huu, Dar es Salaam zikihusisha michezo mbalimbali.

Katika hatua nyingine, TASWA kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Kenya, vimeanzisha program ya ziara ya mafunzo na kubadilishana uzoefu baina ya vyama hivyo viwili, ikiwa katika makundi tofauti ya wahariri/waandishi waandamizi na kundi lingine la waandishi wa habari chipukizi.

Kwa kuanzia wahariri wa habari za michezo 18 au wale wenye uzoefu katika uandishi usiopungua miaka kumi kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wataenda Nairobi kwa ziara ya mafunzo kuanzia Julai 6-9 mwaka huu.

“Tunaamini wakirudi wataendelea kuwa waalimu wazuri kwa wale chipukizi, ambao nao watapata fursa kama hiyo siku za usoni,”.

Young Africans Yaivimbia TFF
Jerry Muro: Tunawafahamu Wanaoleta Figusu Figisu Za Uchaguzi