Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amezitembelea ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) zilizopo mkoani Morogoro.

Akizungumza na Menejimenti na watumishi wa TAWA Balozi Chana amesema ziara hiyo imelenga kufahamu majukumu ya TAWA kama moja ya Taasisi zilizopo chini ya Wizara yake, kujitambulisha na kuzungumza na watumishi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu TAWA.

Kwa nyakati tofauti, katika ziara hiyo Waziri Dkt. Chana ametoa shukrani za dhati kwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake za dhati kwenye kuinua sekta ya utalii nchini ikiwemo uzinduzi wa filamu maalumu ya “Royal Tour” iliyolenga kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini.

Aidha ameagiza Menejimenti na watumishi wa TAWA kuwa tayari wakijipanga kupokea wageni watakao kuja nchini kama matokeo ya filamu ya “Royal Tour”.

“Tuiweke ajenda ya Royal Tour mezani na tuendelee kupanga mikakati ya kupokea wageni hao,” amesema.

Kadhalika, Waziri huyo amewapongeza watumishi wa TAWA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhifadhi rasilimali za Maliasili kote nchini.

Ametoa wito kwa kila mtumishi kuendelea kuwa mfano bora kwenye eneo lake la kazi ili kuendelea kuipa heshima Tanzania kimataifa.

Watumishi wa TAWA

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA, Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis Semfuko, amemuahidi Mhe. Balozi Dkt. Chana kuwa TAWA wataendelea kutoa ushirikiano mkubwa, kuongeza ubunifu na kufanya kazi kwa bidii.

Awali, akitoa taarifa ya utendaji kazi wa TAWA kwa Mhe. Balozi Dkt. Chana, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi- TAWA, Mabula Misungwi Nyanda, amezungumzia masuala mbalimbali yakiwemo majukumu ya TAWA na mafanikio mbalimbali ya Mamlaka.

Baadhi ya mafanikio hayo ni kupungua kwa shughuli za ujangili, kuimarika kwa shughuli za uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori, ugawaji wa vitalu vya uwindaji kwa njia ya mnada wa kielektroniki na uboreshaji wa miundombinu ya utalii kwenye maeneo ya hifadhi.

Hiyo ni mara ya kwanza kwa Waziri Dkt.Pindi Chana kufanya ziara ya kikazi katika ofisi za TAWA tangu alipoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii, Machi 31, mwaka huu.

Dkt. Chana ametoa maagizo haya TAWA
Waandishi wa Habari tusaidie Bara letu- Waziri Nape