Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetupiwa lawama nzito kuhusu sakata la uvushwaji wa kontena 100 katika bandari ya Dar es Salaam bila kukaguliwa na Shirika hilo, ikiwa ni siku moja baada ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuliibua.

Hali hiyo imejitokeza baada ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kudai kuwa wao walifanya kazi yao ipasavyo na kwamba makontena yote yalilipiwa ushuru stahiki.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko alisema kuwa maswali yote yanayohusu kutokaguliwa kwa bidhaa zilizokuwa ndani ya makontena hayo yanapaswa kuelekezwa kwa TBS.

“Hayo waulize TBS, wala hakuna tatizo upande wa TPA,” alisema Mhandisi Kakoko. ”Hatuna haki ya kuwaongelea TBS. Tutakosema tukiingilia mambo ya taasisi nyingine. La msingi ni kwamba sisi tumetekeleza wajibu wetu,” aliongeza.

TBS pia ilirushiwa lawama na Mawakala Forodha Tanzania (Taffa) ambao walidai kuwa suala la ukaguzi wa bidhaa umejaa ukiritimba hali inayocheleweshwa kwa kiasi kikubwa uondoaji wa mizigo.

“Utaratibu wa ukaguzi uliopo sasa unaofanywa na TBS unaleta ukiritimba. Unachukua muda mrefu na kuwafanya wafanyabiashara waone ni kikwazo. Hata vibali vya Mkemia vinakwamisha,” Mtanzania linamnukuu Makamu Rais wa Taffa, Edward Urio.

Akijibu tuhuma hizo zilizoangushiwa kwao, Kaimu Mkurugenzi wa TBS, Dk. Egid Mubofu alisema kuwa suala hilo hivi sasa liko mikononi mwa vyombo vya dola na kwamba watatoa taarifa rasmi baada ya uchunguzi kukamilika.

Aidha, Dk. Mubofu alisema kuwa tayari wafanyabiashara 10 wanaomiliki baadhi ya makontena hayo wamewasiliana na Shirika hilo Alisema watatu kati yao walifika ofisini kwake na saba walipiga simu.

Kwa upande wake Waziri Mwijage alisema kuwa analifanyia kazi suala hilo kwa kufanya ufuatiliaji yeye mwenyewe na kwamba atatoa taarifa kamili kupitia mkutano na waandishi wa habari.

”Nilisema suala hili nalifuatilia mwenyewe kuanzia saa 12 asubuhi. Niko bandarini, niko mtaani, niko nawatafuta marafiki wangu wa zamani wote wenye taarifa za kutosha. Kwahiyo mkutano ujao na waandishi wa habari nitatoa taarifa rasmi,” Mwijage anakaririwa.

Butiku: Wanasiasa wote wanababaisha kuhusu kanuni hii ya Mwalimu Nyerere
Manispaa ya Ilala Wamuenzi Baba wa Taifa kwa Kufanya Usafi