Bodi ya Shirika la Viwango Tanzania TBS imeiagiza Menejimenti ya Shirika hilo kuhakikisha inamsimamia mkandarasi anayejenga kituo cha ukaguzi wa magari yanayoingizwa nchini kutoka nje ya nchi, ili kituo hicho kianze kazi mapema mwezi Julai mwaka huu kama ilivyoagizwa na Serikali.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Othman Chande Othman ametoa agizo hilo alipoongoza wajumbe wa Bodi yake kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho katika bandari ya DSM, na kuonesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo na hivyo kutia mashaka iwapo kitakamilika katika muda uliopangwa.

Aidha amesema ziara hiyo ni ufuatiliaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa katika bandari ya DSM hivi karibuni ambapo pamoja na mambo mengine alitoa maagizo ya kutaka kituo hicho cha ukaguzi wa magari kikamilike mwishoni mwa mwezi ujao.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dkt. Yusuf Ngenya pamoja na kuahidi kutekeleza maagizo ya Bodi, amesema kituo hicho kitakapokamilika, kitaongeza kasi na ufanisi katika ukaguzi wa magari, ambapo magari manane yatakuwa yanakaguliwa kwa wakati mmoja.

TBS kkwa sasa inaendesha ukaguzi wa magari katika yadi ya mabasi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) hadi ujenzi unaoendelea wa kituo kipya utakapokamilika.

Bashungwa atoa siku 30 TARURA barabara ya Golani
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Mei 15, 2022