Mamlaka ya mawasiliano Tanzania TCRA imewataka wauzaji wote wa simu za mikononi wanaoingiza mizigo kutoka nje ya nchi kuhakikisha wanaingiza simu zinazokidhi viwango na zimehakikiwa kwa mujibu wa shirika la viwango nchini.

Kauli hii imekuja ikiwa imebaki siku moja ili Mamlaka ya mawasiliano nchini kutekeleza agizo la serikali la kuzima simu zote bandia ifikapo juni 16 lakini bado mamlaka hiyo pamoja na wadau mbali mbali wameona changamoto zinazohitaji kutatuliwa.

Kaimu Mkurugenzi mkuu,Mhandisi James Kilaba amezungumza na wanahabari leo jijini Dar es salaam na kusema uaminifu mdogo kwa baadhi ya wauzaji wa simu na uelewa mdogo kwa baadhi ya wananchi bado ni changamoto hasa katika kuitikia wito wa kuhakiki simu katika kipindi hiki cha mpito.

Aidha Bw. kilaba amefafanua kuwa simu zitakazozimwa siku ya kesho ni pamoja na zile zilizobadilishwa (flash) namba tambulishi ya simu pamoja na vifaa vya simu haswa kwa kuzingatia tendo hilo ni ukiukwaji wa sheria na adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka kumi au faini  isiyopungua milioni 30 au vyote kwa pamoja.

Ameongeza kuwa wafanyabiashara wanahitajika wawe na leseni ya mamlaka ya mawasiliano kwa mujibu wa sheria ili kufanya kazi zao huku akisisistiza hakuna uwezekano wa simu bandia kufanya kazi kwa njia yoyote ile baada ya kuzimwa.

Akielezea faida za kusajili simu Bw.Kilaba amesema ni ili kudhibiti wizi wa simu nchini,kuhimiza utii wa sheria na kujenga misingi ya matumizi ya simu halisi kwani mtumiaji ataweza kutambua kama simu anayotumia ni bandia au laa.

 

Video: Jeshi la Polisi limepata Milioni 61650 ndani ya siku 10
Fastjet kutoa misaada kwa watoto yatima siku ya mtoto wa Afrika