Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imevitaka vyombo vya Habari kuzingatia maadili katika utendaji wao wa kazi, hatua itakayosaidia kuongeza wigo wa wafuatiliaji wa Habari zenye uhakika na zisizo na walakini.

Akizungumza katika ziara ya TCRA kutembelea ofisi za DAR24 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Habbi Gunze amesema ubunifu katika kutenda kazi husaidia kutengeneza wasifu mzuri wa kituo kwa kuakisi uhalisia wa matukio ya kihabari yanayozingatia maudhui.

Amesema zipo changamoto katika utafutaji na uibuaji wa Habari zenye mashiko, lakini uzingatiaji wa maadili huleta utofauti wa mapokeo baina ya chombo kimoja na kingine na hivyo kwamba ubora wa kazi huleta ufanisi zaidi na kupata taswira chanya.

“Mnaweza kujitofautisha na wengine kwa kuzingati Habari zinazozingatia maudhui na zilizo sahihi, lakini uibuaji wa hoja zinazogusa jamii utawafanya ninyi DAR24 kujitofautisha sokoni na hivyo kuweza kuwa zaidi ya wengine,” amesema Gunze.

Kuhusu changamoto za vyombo vya Habari upande wa mitandao ya kijamii, Gunze amesema hoja zenye ukweli katika matokeo ya ukusanyaji wa maoni juu ya nini kifanyike ili kuziwezesha kufanya vizuri utasaidia kuleta maboresho.

Amesema, “kumekuwa na malalamiko ya vyombo hivi vya online kuwa na ugumu katika kupata matangazo, kutokana na kasumba ya baadhi ya wafanyabiashara kuchagua wapi liende tangazo lakini hii inatokana na ubora wa kazi, kujituma na uibuaji wa habari zinazomfanya mfanyabiashara kuona bidhaa yake ikitangazwa na chombo hiki basi itawafikia wengi.”

Akijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Mamlaka ya TCRA, Meneja Msaidizi wa DAR24, Abel Kilumbu amesema mbali na mambo mengine Online Media zimekuwa zikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutoaminika na baadhi ya wanajamii na hata wafanya biashara ambao wangeweza kusaidia maisha ya vyombo hivyo

“Hakuna imani kwa vyombo hivi na hata wafanya biashara hawachukulii online Media kama ni eneo zuri la kutangazia biashara zao ni wachache tu ambao wananufaika na hili lakini wengi wetu hali ni tufauti na tunajiendesha kwa hasara,” amefafanua Kilumbu.

Ameongeza kuwa, “Nadhani kuna haja ya kusaidiwa katika upande huu maana kuna dharau kidogo tangazo la bei kubwa mtu anataka umtangazie kwa pesa ambayo hailingani na hitaji lake na ikizingatiwa kwamba kwenye online matangazo yanaishi sio kama upande wa ‘Traditional Media’ huku mika hata 50 tangazo lake akilitafuta linakuwepo.”

Awali, akiongea katika kikao kilichofanyika mara baada ya kupokea ugeni huo, Mtendaji Mkuu Msaidizi wa Data Vision, William Kihule alifafanua juu ya maudhui yanayochapishwa na kituo hiki ambayo yameegemea katika uibuaji wa mambo mbalimbali yanayogusa jamii moja kwa moja na kuleta matokeo chanya.

“Katika tafiti mbalimbali za DataVision ambazo tulizifanya maeneo mbalimbali tulikuwa tukikutana na mambo mengi ya kijamii, hili lilitufanya tuanzishe DAR24 ili chombo hiki kiwe daraja kati ya jamii na watunga sera na Serikali kiujumla, lengo ni kufikisha ujumbe, kuibuia mambo mbalimbali na kutafuta suluhisho kwa ushirikiano na mamlaka.

Kihule amesema, pamoja na mambo mengine pia wanalenga kufanya maboresho katika utendaji wa DAR24 ikiwemo kuzingatia maudhui, kuwa na wafanyakazi wenye taaluma watakaosaidia kufikia malengo ya kituo na wenye uwezo wa kufanya kazi kwa kuzingatia sera za kituo na mamlaka za kiserikali ikiwemo miongozo ya TCRA.

Hata hivyo, akijibu baadhi ya hoja za kituo, Mwenyekiti huyo wa Kamati ya maudhui ya TCRA, amewashauri Viongozi waandamizi wa DAR24 kufikiria namna ambavyo wanaweza kujiongezea ufanisi, ikiwemo kukikuza chombo hicho kama ilivyo kwa vituo vingine vya Kidigitali kutokana na mfumo mzuri ulioanishwa kiutendaji na ratiba ya vipindi husika kitu kitakachosaidia kufikia maono.

Amesema, uzingatiaji wa maudhui ikiwemo kufuata miongozo ya TCRA iliyopo kwenye tovuti inaweza kusaidia kuboresha mambo mbalimbali ambayo ni changamoto kwa vituo vingi, huku akipongeza uwekezaji uliofanywa na Data Vision kwenye chombo cha Habari cha DAR24.

Nusu ya watoto wenye UKIMWI hawapatiwi matibabu
Kesi unyanyasaji kingono zaongezeka kwa asilimia 218