Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewafungulia milango muhimu vijana wabunifu katika Teknolojia, Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuwapa uwezeshaji uliokuwa unakwamisha ubunifu miaka yote nchini, imebainika.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabir Bakari amesema Serikali ya Tanzania imeamua kutoka rasilimali kwa vijana wabunifu katika sekta ya TEHAMA. Rasilimali za mawasiliano zinazotolewa na TCRA kwa ajili ya vijana wabunifu kufanya majaribio ni pamoja na misimbo ya USSD, yaani rasilimali-namba.

Amesema kuwa hizi ni namba maalum zinazotumika kumpa mbunifu fursa ya kusambaza teknolojia aliyoibuni ndani na nje ya nchi. Pia TCRA kwa sasa wanato kikoa (domain) cha dot tz (.tz) na masafa ya mawasiliano.

Fursa zilizotolewa zinahitaji kijana kuwa na ubunifu kama mtaji wake na vifaa vya gharama nafuu vya TEHAMA kama vile kompyuta mpakato na simu ya kiganjani au vifaa rununu pendwa kama vile kishikwambi kukamilisha ubunifu wake.

Hata hivyo, Dk. Jabir, amesisitiza kuwa vijana wabunifu na wavumbuzi wa programu mbalimbali za kidijitali sasa wanaweza kujitokeza kupata rasilimali hizo zitakazowawezesha kupata fursa ya kutengeneza ajira kujiletea kipato na kutatua changamoto mtambuka za jamii.

“Tumejipanga kuhakikisha wabunifu wapya hasa wa sekta ya TEHAMA wanaoweza kutatua changamoto za jamii yetu wanapata rasilimali hizi za mawasiliano, ili washiriki katika uchumi wa kidijiti,” amesisitiza Dkt. Jabir.

“Tuna utaratibu wa kutoa rasilimali hizi kwa muda wa miezi mitatu; ambazo tunatoa [kwa mbunifu] baada ya kuidhinishwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia ambayo hujiridhisha kubaini kama wazo la kibunifu linakidhi kufanyiwa majaribio na hapo ndipo tunatoa rasilimali za masafa au misimbo ya namba fupi kwa muda wa majaribio wa miezi mitatu,” amebainisha Dkt. Jabiri.

Mbali na fursa zinazotolewa na TCRA, COSTECH na Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa wabunifu wa TEHAMA nchini, Tume ya TEHAMA (ICTC) nayo haipo nyuma.

Tume hii inaendesha program ijulikanayo kama Softcentre inayotoa msaada wa moja kwa moja kwa kampuni changa (Startups), ikiwa ni kutekeleza mpango wa mapinduzi ya kidijitali unaolenga kutatua tatizo la ajira na kukuza ubunifu wenye tija.

Tume hii pia imekuwa ikiendesha Tuzo za kampuni changa (ICT Startups Awards) zinazotumia TEHAMA kutatua changamoto mbalimbali katika jamii kwa bunifu zenye tija. Mashindano kwa kampuni changa yanaendeshwa na Tume ya TEHAMA kwa malengo ya kutambua wabunifu nchini na kuwawezesha.

TCRA huratibu vikao vya mashauriano na wadau wakuu wanaojishughulisha na ubunifu kujadili masuala yanayohusu fursa na changamoto za programu za ubunifu wa TEHAMA kukua na jinsi TCRA inavyoweza kuweka mazingira wezeshi ikizingatiwa kwamba Mamlaka hiyo ni taasisi wezeshi katika sekta pana ya Mawasiliano.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeondoa malipo ya ada ya maombi na usajili wa leseni wa rasilimali hizo kwa ajili ya wabunifu wenye nia ya kubuni suala lolote litakalorahisisha mazingira ya kawaida ya kila siku ya mwananchi.

Pia, watoa huduma za mawasiliano ya simu kwa kuwaunganisha wabunifu hawa bure kwenye mitandao yao wakati wa kipindi cha majaribio.

Wabunifu wanaotaka kutumia fursa hii wanaweza kuwasiliana na Dawati la Huduma la TCRA kupitia namba 0800008272 au kutembelea tovuti www.tcra.go.tz

UDSM, IMS kushirikiana na Serikali Uchumi wa buluu
Picha: Rais Samia aongoza kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri