Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa onyo kali kwa vituo vya redio vya Magic FM na Radio Free Afrika kwa kosa la kukiuka maagizo ya serikali na kusoma kwa kina habari za magazetini badala ya vichwa vya habari.

Kamati ya Maudhui ya TCRA imeeleza kuwa Magic FM ilifanya kosa hilo kwa makusudi Mwezi Januari kupitia kipindi chake cha Morning Magic.

Kadhalika, Radio Free Afrika wamedaiwa kufanya kosa hilo kupitia kipindi chake cha magazeti cha asubuhi. Imeelezwa kuwa mtangazaji wa kipindi hicho, kwa makusudi alisoma habari za magazeti kwa kina badala ya vichwa vya habari.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Valeriani Msoka amewaambia waandishi wa habari kuwa baada ya kuwahoji kwa nyakati tofauti kamati haikurishishwa na hoja za utetezi wao.

“Kamati haikurishishwa na utetezi kutoka pande zote mbili, sababu zao hazikuwa na mashiko, kwahiyo tunawapa onyo kali kutorudia makosa hayo tena,” Msoka amewaambia waandishi wa habari.

Aidha, Kamati hiyo imevitaka vyombo hivyo vya habari kuhakikisha vinafanya maandalizi ya kutosha pamoja na kuwapa elimu watangazaji wake kuhusu maagizo ya Serikali.

Mwaka 2017, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliagiza vyombo vyote vya habari kutosoma kwa kina habari katika magazeti bali visome vichwa vya habari pekee, lengo likiwa kuyasaidia magazeti kuendelea kufanya biashara ya kuwauzia watu maudhui yake.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Aprili 16, 2019
JPM akutana na wabunge wa CCM Dodoma

Comments

comments