Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza kuvifutia usajili vyuo tisa kwa sababu za kushindwa kutimiza vigezo na masharti ya kutoa mafunzo.

Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Profesa Charles Kihampa amewaambia waandishi wa habari leo, Januari 21, 2020 jijini Dar es Salaam kuwa baada ya kufanya kikao na wamiliki wa vyuo hivyo kuhusu mazingira ya utoaji elimu yasiyoridhisha, wamiliki hao waliomba kusitisha kutoa mafunzo hivyo wamefutiwa usajili.

Profesa Kihampa alieleza kuwa ingawa Tume hiyo imekuwa ikitoa ushauri wa jinsi ya kuboresha mazingira ya utoaji wa mafunzo katika vyuo hivyo, imebainika kuwa havitaweza kufikia ukidhi unaohitajika.

“Licha ya Tume kutoa mafunzo ya namna mbalimbali za kuboresha mazingira ya kufundisha na kufundishia, pamoja na muda wa kufanya maboresho kwenye maeneo mbalimbali kwa miaka mitatu, baadhi ya vyuo havikufanikiwa,” amesema Profesa Kihampa.

Vyuo vilivyofutiwa usajili ni pamoja na Chuo Kikuu Kishiriki Cha Askofu Mkuu Yacobo (AJUCO), Chuo Kikuu Cha Kumbukumbu ya Kardinali Rugambwa (CARUMUCO), Chuo Kikuu cha Theofilo Kisanji (Teku-Dar es Salaam), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania Kituo cha St. Marks na Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta cha Kilimo Tawi la Arusha (JKUA).

Vingine ni Chuo Kikuu cha Josiah Kibira (Kagera), Mount Meru (Arusha), IMTU (Dar es Salaam), pamoja na Chuo Kikuu cha Bagamoyo (Pwani).

 

Rais Magufuli afanya uteuzi leo
Virusi vya ugonjwa uliolipuka China vyazua hofu kusambaa duniani, WHO kukutana kwa dharura