Waziri wa kilimo Japhet Hasunga amezindua mfumo wa njia ya simu ‘T-hakiki’ kwaajili ya kuhakiki pembejeo za kilimo.

Uzinduzi wa mfumo huo unaolenga kuwakomboa wakulima katika mapambano dhidi ya mbegu na viuatilifu feki, umefanyika katika maadhimisho ya nanenane mwaka 2020 ndani ya Banda la Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Akizungumza katika uzinduzi huo, Hasunga amesema uuzaji wa pembejeo feki za kilimo unasababisha athari kubwa kijamii na kiuchumi.

“Matokeo yake yamesababisha changamoto nyingi kwa sekta ya kilimo ambayo ndiyo sekta muhimu inayochangia kuongeza tija kwenye uchumi wa Taifa, kwa maana hiyo huduma hii ni mkombozi halisi kwa wakulima wetu” amesema Hasunga

Hata hivyo huduma hiyo imetokana na ubunifu wa Shirika la mawasiliano Tanzania (TTCL), kwa kushirikiana na kampuni ya Quincewood Group Limited na wadau wa sekta ya kilimo kama vile Taasisi ya kudhibiti ubora wa mbegu Tanzania (TOSCI) na Taasisi ya utafiti  na udhibiti wa viuatilifu (TPRI), ambao wamekuja na suluhisho la kiteknolojia kukomesha matumizi ya pembejeo feki. 

Naye Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya utafiti wa viuatilifu ukanda wa Tropiki (TPRI), Dk. Margaret Mollel amesema ubunifu huo umeenda sambamba na malengo ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kuleta mapinduzi kwenye sekta ya kilimo.

Akifafanua namna mfumo huo unavyofanya kazi, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba  amesema T- Hakiki ni mmfumo wa simu ya mkononi ambao ni mkombozi kwa sekta ya kilimo nchini.

“T-Hakiki ni mfumo wa njia ya simu ambapo unabofya *148*52# na kuingiza namba za siri zilizo kwenye vifungashio vya mbegu au kwenye chupa za viuatilifu ili kuthibitisha uhalisia wa pembejeo. Huduma ya T-Hakiki inapatikana katika mitandao yote ya simu na ni bure,” alisema Waziri Kindamba 

Makamu wa Rais atahadharisha rushwa Uchaguzi Mkuu
Mahakama yabariki miaka 20 jela kwa kigogo wa dawa za kulevya