Serikali kupitia wizara ya Maliasili na Utalii imejipanga kuanzisha mfumo maalum wa kuwavisha tembo kola zijulikanazo kama visukuma mawimbi ili kutambua mwelekeo wao kwa ajili ya kuwazuia kuingia katika makazi ya watu.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema hayo katika ziara yake ya kusikiliza changamoto za wanyama wakali na waharibifu iliyofanyika katika Kijiji cha Goha, Kwalukonge na Kweisewa, Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga.

Naibu Waziri Mary Masanja akitoa ufafanuzi

“Makundi ya tembo ambayo yanaonekana kuzagaa tutayaingiza kwenye mtambo na tembo viongozi tutawafunga kola zijulikanazo kama visukuma mawimbi na tutayafuatilia yameenda wapi,” amesema Masanja.

Amesema kupitia njia hiyo Askari wa Uhifadhi wataweza kuwafuatilia kwa karibu na endapo kundi lolote la tembo litakuwa na mwelekeo wa kuingia kwenye makazi ya watu, watalizuia kabla ya madhara kutokea.

Aidha, ameahidi kujenga kituo cha Askari wa Uhifadhi katika vijiji hivyo ili kurahisisha zoezi la kuzuia uharibifu unaofanywa na tembo.

Pia, amesema Serikali imejipanga kutoa elimu ya namna ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu ambapo vijana watafundishwa mbinu mbalimbali.

Kuhusu kifuta jasho/machozi ameahidi kuwa Serikali itawalipa waathirika wote ifikapo mwezi wa nane mwaka huu.

Awali, mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Goha, Mohamed Ramadhani amesema kuwa tembo wamekuwa wakivamia mashamba kila ifikapo saa 4 usiku na hivyo kuiomba Serikali kuwapeleka Askari wa Uhifadhi ili kuwa kuwasaidia wananchi kukabiliana na adha hiyo.

Naye, Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mzava ameiomba Serikali kuangalia namna bora ya kuweka uzio ili kuzuia tembo , kujenga kituo cha askari wa wanyamapori na pia kuelimisha wananchi kuhusu mbinu za kupambana na tembo wanapovamia makazi yao.

Ziara hiyo ni mwendelezo wa ziara za kusikiliza changamoto za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.

Kocha Zoran Maki ang'oa watatu Simba SC
Habari kuu kwenye magazeti ya leo Julai 29, 2022