Kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi, Kanali Mstaafu Issack Mwisongo, amezitolea majibu tetesi zilizoenea kupitia mitandao ya kijamii na vijiwe maarufu vya mijadala ya kisiasa kuwa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alimkataa waziri mkuu wa zamani, Edward Lowasa.

Akizungumza jana katika mkutano wa Edward Lowasa mjini Morogoro uliokuwa sehemu ya kampeni ya kutafuta wadhamini ili kumuwezesha kupata ridhaa ya kuwania nafasi ya urais kupitia CCM, Mwisongo alisema kuwa hajawahi kumsikia Mwalimu Nyerere akitoa kauli hiyo katika kikao chochote cha chama.

“Mimi nimekuwa katika vikao hivyo vyote na kama Nyerere ukikosea au hakutaki, alikuwa anakukutaa waziwazi na pia unatangazwa kwenye vyombo vya habari,” alisema Kanali huyo mstaafu.
Aliwataka wajumbe wa vikao vya maamuzi vya CCM kutofanya makosa huku akiweka wazi kuwa NEC ndiyo yenye nguvu zaidi.

Naye mwenyekiti wa CCM wilaya ya Morogoro Mjini, Fikiri Juma alimtaka Lowasa kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa hata katika semina kwa wenyeviti iliyoandaliwa na kuratibiwa na chama hicho, walisisitizwa kuhakikisha wanachagua viongozi wanaokubalika zaidi ndani ya chama.

“Haki isipotendeka katika vikao vya maamuzi sisi bado tupo pamoja na wewe,” alisema.
Mbunge wa Munduli, Edward Lowasa ambaye ni mmoja kati ya makada zaidi ya 40 wa CCM waliochukua fomu za kuwania nafasi ya kugombea kiti cha urais kupitia chama hicho amepata wadhamini zaidi ya 870,000 katika mikoa 31 ya Tanzania.Lowasa alitumia fursa hiyo aliwashukuru wanachama wa CCM waliojitokeza kumdhamini katika mikoa yote.

Mwisho wa kurejesha fomu kwa wagombea wote ni July 2, mwaka huu.

Azam FC Kushusha Wachezaji Sita Kufunika CECAFA
Video Mpya: Ali Kiba – Chekecha Cheketua