Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania TFDA imeweka mfumo maalum wa udhibiti wa usalama wa
chakula kinachozalishwa ndani ya nchi na kile kinachoingizwa kutoka nje ili kuwahakikishia afya bora
kwa walaji.

Mfumo huo ni kufanya tathmini ya vyakula vilivyofungashwa, kusajili maeneo na kutoa vibali vya
biashara za vyakula, kufanya ukaguzi wa vyakula katika soko pamoja na ukaguzi wa maeneo ya
kusindikia, kuhifadhia na kuuzia vyakula.

Hayo yamesemwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Adam Fimbo wakati akifungua Semina ya siku mbili kwa waandishi wa Habari iliyofanyika Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani, ambapo amesema kuwa mfumo huo pia unalenga kuchunguza sampuli za vyakula katika maabara.

“Ndugu zangu Waandishi wa Habari, naomba muufahamishe Umma kuwa mfumo huu unahakikisha kila Mtanzania anatumia chakula salama, na tunaanzia mipakani na kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini” amesema Fimbo.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa chakula wa TFDA, Moses Mbambe amesema kuwa umuhimu wa usalama wa chakula Nchini Tanzania unapewa kipaumbele kwa kushirikiana na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo kupitia kikao chake cha Disemba 28 2018 ilipitisha siku ya usalama wa Chakula Duniani kuwa Juni 7 ya kila mwaka ambapo kwa mara ya kwanza Duniani kote siku hiyo ilianza mwaka huu wa 2019.

Kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani WHO takribani Watu Milioni 600 Duniani sawa na Mtu mmoja kati ya watu 10 huugua kila mwaka kutokana na kula chakula kisicho salama na kati yao watu 420,000 hufariki na huku watoto wakiwa 125,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano ambapo kwa Bara la Afrika zaidi ya watu milioni 91 wanakadiriwa kuugua huku watu 137,000 hufariki dunia kila mwaka.

Wanaowachapa makofi akina Mama wakati wa kujifungua Waonywa
video: Tanzania, DRC Wakubaliania maeneo tisa nyeti, Muujiza mbegu za maboga kwa kinababa