Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imesema kuwa katika kipindi Cha Miaka mitatu imeweza kufanya mambo mbalimbali ya udhibiti wa usalama, ubora na usalama wa bidhaa za ndani na nje ya nchi ikiwemo kutambulika kimataifa kwa kuzingatia  viwango vya Kimataifa vya ISO 9001: 2015.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Adam Fimbo wakati akitoa ripoti ya miaka mitatu ya Mamlaka hiyo  wakati wa ziara maalum ya Maafisa Mawasiliano na habari wa Wizara ya Afya na taasisi zake katika kampeni maalum ya ‘Tumeboresha Sekta ya Afya’ inayolenga kueleza mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitatu.

“Kutokana na kuwa na mifumo thabiti ya udhibiti wa ubora,  usalama na ufanisi wa dawa, mnamo Mwezi Desemba 2018, TFDA imetambulika kufikia ngazi ya tatu (Maturity Level 3) ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya ubora wa mfumo wa udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vipodozi, ambapo hatua hii imeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufikia hatua hii,”amesema Fimbo

Aidha, ameeleza kuwa, TFDA katika mikakati yake hiyo imeweka mifumo na taratibu za ndani za utoaji huduma na utendaji bora ili kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya ISO 9001:2015 kwa huduma za kawaida na ISO 17025:2005 kwa huduma za maabara.

Pia amesema kuwa huduma za TFDA hutolewa kwa kuzingatia viwango vya Mkataba wa Huduma Wateja kama ulivyorejewa mwaka 2016.

Hata hivyo, ameongeza kuwa, TFDA katika kipindi cha miaka mitatu (2015/16 – 2017/18), imeweza kusajili jumla ya maeneo 25,630 ya biashara za bidhaa zinazodhibitiwa ikiwa ni pamoja na maeneo 9,000 yaliyosajiliwa mwaka 2016/17 na maeneo 5,606 mwaka 2015/16, hii ikiwa ni sawa na ongezeko la 60.5%.

Mwanamke ajitolea kulea sokwe yatima
Video: Mnyika amvaa Spika Ndugai, Maajabu 8 ya Zanzibar